YANGA YAIPIGA MKWARA SIMBA KUELEKEA DABI NOVEMBA 7, YAWAITA MASHABIKI

UONGOZI wa Yanga umewataka mashabiki wake kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa Novemba 7 kushuhudia namna watakavyotoa burudani kwa wapinzani wao Simba kwenye dabi ya Kariakoo.

Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 23 baada ya kucheza mechi 9 wanakutana na mabingwa watetezi Simba ambao wapo nafasi ya tatu na pointi zao ni 19.

Mechi zao zilizopita hivi karibuni timu hizo zilikuwa na matokeo tofauti ambapo Yanga ambao ni wenyeji walisepa na pointi moja Uwanja wa Gwambina Complex kwa kulazimisha sare ya bila kufungana huku Simba ikitoka kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz ameweka bayana kuwa walikuwa wanawatamani wapinzani wao Simba tangu Oktoba 18 ila mambo yalishindikana kutokana na ratiba kubadilishwa na sasa wanakwenda kukutana Novemba 7.

“Unajua sisi Yanga hatuna mchezo kwenye suala la kusaka pointi tatu, kikosi chetu ni bora na kinatoa burudani hivyo mashabiki ninawaomba wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kushuhudia burudani.

“Kwa kuwa tuliwakosa Oktoba 18 basi kazi itaendelea pale kwa Mkapa Novemba 7 hatuna mashaka tuna kikosi chenye wachezaji wazuri na wanajua majukumu yao, tukutane kwa Mkapa,” amesema.

Mechi ya mwisho ya watani wa jadi msimu uliopita Machi 8, Simba ilinyooshwa bao 1-0 lilipachikwa kimiani na Bernard Morrison ambaye kwa sasa ni mali ya Simba.

Kwenye mchezo huo atakuwa jukwaani akishuhudia mabosi zake wa zamani wakimenyana na mabosi wake wapya kwa kuwa amefungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso.

Kwenye mchezo huo Simba ilitulizwa kwa bao 1-0 Uwanja wa Uhuru na ameshakosa mchezo mmoja dhidi ya Kagera Sugar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *