Waziri wa Ujerumani aionya Iran

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Heiko Maas ameitolea mwito Iran kuacha kuingilia migogoro ya ndani katika ukanda huo.

Tamko la waziri Maas amelitowa wakati wa ziara yake nchini Jordan leo Jumatatu. Baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Jordan Ayman Safadi, Maas amesema wamekubaliana ikiwa Iran inataka kumaliza migogoro lazima iache kujiingiza kwenye migogoro ya eneo hilo ikiwemo Iraq.

Waziri wa mambo ya nje wa Jordan, Safadi amesema kwamba kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS bado ni kitisho katika ukanda huo.

Jordan ni mshirika muhimu wa nchi za Magharibi katika vita dhidi ya kundi hilo la kigaidi na kwa sasa inawahifadhi zaidi ya Wasyria milioni moja waliokimbia vita nchi mwao.

Waziri Maas pia amepanga kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani walioko kwenye kambi ya Al Azraq iliyoko kilomita karibu 90 kutoka mashariki mwa mji mkuu wa Jordan, Amman.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *