Waziri Biteko atembelea GGML “tumekusanya Bilioni 400 Geita mmeongeza”

Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameipongeza Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya dhahabu – Geita (GGML) kwa kuwa mdau wa mfano katika kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Geita.

Biteko ametoa kauli hiyo jana katika ziara fupi aliyoifanya mkoani Geita na kukagua miradi inayotekelezwa na Kampuni ya GGML chini ya mpango wake wa kusaidia jamii (Corporate Social Responsibility) katika Mji wa Geita.

Aidha, alisema lengo la Serikali ni kuona maisha ya watu katika maeneo yote yenye rasilimali madini, ikiwemo Geita yanabadilika kiuchumi.

“Nimefurahishwa na namna ambavyo Serikali katika Mkoa wa Geita inavyosimamia ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye sekta ya madini. Tayari tumeshafikia lengo la kukusanya zaidi ya Sh bilioni 400 kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2020 kutoka kwenye sekta hii, na sehemu kubwa ya makusanyo haya imetoka Geita, hususan GGML.

“Inatia moyo sana kuona kwamba sekta hii sasa inachangia zaidi ya asilimia 5 ya uchumi wa nchi yetu. Lengo ni kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025,’’ alisema Biteko.

Mojawapo ya miradi ambayo ilikaguliwa na waziri huyo katika ziara yake ni ujenzi wa Kanda maalumu ya uwekezaji ”Special Economic Investment Zone” ambao utasimamiwa na Mamlaka ya ukanda maalumu wa Uwekezaji (EPZA) na Halmashauri ya Mji wa Geita.

Pia alitembelea miradi mingine ya kimkakati inayofadhiliwa na GGML, ikiwemo ujenzi wa Soko Kuu la Geita Mjini na soko la Katundu.

Aidha, Makamu wa Rais anayeshughulikia Maendeleo Endelevu katika Kampuni ya GGML, Simon Shayo alisema utekelezaji wa miradi ambayo imetembelewa na waziri Biteko ni sehemu ya mpango wa mwaka 2018/19 unaoenda sambamba na mojawapo ya tunu za kampuni hiyo inayoelekeza kwamba jamii inayozunguka shughuli zake sharti ifaidike kwa uwepo wake.

Alisema GGML ambayo ni sawa na kampuni-raia inawajibika ipasavyo kwa jamii kwani hutumia Sh bilioni 9.2 kila mwaka kugharimia miradi ya jamii katika mkoa wa Geita na kuifanya kampuni hiyo kuwa ya kipekee kutokana na mchango mkubwa inayotoa kusaidia jamii.

“Kama Kampuni-raia ndani ya Tanzania, GGML iliyoko chini ya AngloGold Ashanti itaendelea kuunga mkono na kusaidia jamii zinazotuzunguka. Utekelezaji wa miradi ya CSR na shughuli zingine kama hizo ni ushahidi wa wazi kwamba kampuni, serikali na jamii zikifanya kazi pamoja zinaweza kuboresha maisha ya watu kupitia uwekezaji endelevu katika miundomuni ya biashara na huduma.

“Tunataka kuona maisha ya mtu wa kawaida katika jamii yetu yakiwa bora zaidi kupitia uwekezaji endelevu wa Kampuni yetu” alisema.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2018, GGML iliwezesha utekelezwaji wa miradi kadhaa kupitia mpango wake wa kuwekeza katika jamii.

“Miradi hii inajumuisha; uwekaji wa taa za barabarani katika mji wa Geita, ujenzi wa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ujenzi wa soko la kisasa Geita mjini, umaliziaji wa majengo zaidi ya 600 ya afya na elimu na ujenzi kamili wa shule tatu mpya na vituo vya afya vinne.

“Pia GGML imetenga kiasi cha Sh bilioni 18 kwa ajili ya miradi mingine kama hiyo katika kipindi cha kati ya mwaka 2019/20 na 2020/21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *