Wayemeni zaidi ya milioni 20 wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na corona

Shirika la Programu na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limetangaza kuwa, zaidi ya Wayemeni milioni 20 wanasumbuliwa na njaa ya muda mrefu na wamo katika hatari ya kupatwa na virusi vya corona.

Takwimu za karibuni kabisa zinaonyesha kuwa, Wayemeni 419 wamepatwa na virusi vya corona na 95 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo.

Ripoti hiyo ya UNDP imesema kuwa Wayemeni milioni 20.1 wanasumbuliwa na njaa na kuna uwezekano mkubwa wakapatwa na virusi vya corona.

Awali ripoti ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilikuwa limetangaza kuwa, virusi vya corona vinasambaa bila ya kutambuliwa baina ya Wayemeni na kwamba vitasababisha maafa makubwa katika nchi hiyo ambayo inasumbuliwa na njaa, utapiamlo na ukosefu wa huduma za tiba.

Yemen inaendelea kushambuliwa na Saudi Arabia na washirika wake tangu mwaka 2015 na sehemu kubwa ya miundombinu ya nchi hiyo imebolewa kabisa. Maefu ya raia wa Yemen wameuawa katika mshambulizi hayo na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *