Wanne Wakamatwa Na Dawa Za Kulevya Aina Yaheroin Shinyanga

Wakazi wanne wa Manispaa ya Shinyanga wanashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani Shinyanga wakiwa na dawa za kulevya aina ya Heroine Pinchi 8.
Kwa Mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo Aprili 20 mwaka huu na Kamanda wa Polisi Mkoani humo ACP Debora Magiligimba alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Aprili 19 mwaka huu katika mtaa wa Majengo kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga.
Kamanda Magiligimba amewataja watu ambao ni pamoja na Hassani Ibrahimu (22) mkazi wa Majengo,Juma Omary(26) Mkazi wa Ngokolo,Abdalah Hemed (23)mkazi wa Majengo na Chiku Tungu (57)mkazi wa Majengo.
“Askari walipata  taarifa za kiintelejensia kuhusiana na uwepo wa watu wenye dawa hizo za kulevya ndipo walifika nyumbani kwa Chiku Tungu na  kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo,”alisema Kamanda Magiligimba.
Alifafanua kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na dawa hizo ambazo ni  pinchi 08 za heroine pamoja na rizla, kitezo, kigae na kisu kimoja na bado wanaendelea kuhojiwa na baadae watafikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo Kamanda Magiligimba alitoa  wito kwa wananchi kuendelea  kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutokomeza uuzwaji, utumiaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya ili kuikinga jamii dhidi ya madawa hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *