Wakulima Babati watakiwa kugomea vipimo visivyo halali.

Na Mwandishi wetu, Babati
WAKULIMA wametakiwa kugomea vipimo visivyo rasmi vya magunia na madebe wakati wa kupima mazao yao kwani vinawanyonya hivyo watumie mizani ili kuepuka kudhulumiwa haki zao.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, John Nchimbi aliyasema hayo kwenye mkutano wa 13 wa Mtandao wa vikundi vya wakulima (Mviwata) mkoani Manyara.
Nchimbi alisema wakulima wanapaswa kutambua kuwa vipimo vya ubabaishaji na wizi vya magunia na madebe hayapaswi kutumika kwa sasa kwa hiyo wagomee hilo na kusisitiza kuwepo kwa vipimo kwa kilo.
Alisema serikali itawaunga mkono kwenye hilo endapo wao wenyewe watakuwa na msimamizi mkali wa kuepuka kunyonywa mazao yao ili wakulima wapate tija na kuepuka kudhulumiwa.

“Mviwata haiwezi kukulinda wala serikali haitaweza kukusaidia endapo mkulima mwenyewe hautagomea vipimo vya wizi na ubabaishaji dhidi ya mazao ya mkulima.

Hata hivyo, alisema baadhi ya wakulima wanaweza kuwa vikwazo kwa wenzao kwa kukubali kutumia vipimo vya magunia na madebe kutokana na tamaa ya muda mfupi badala ya kuwa na msimamo.
Mratibu wa Mviwata mkoani Manyara, Martin Pius alisema wamekuwa karibu na wakala wa vipimo Tanzania juu ya kutumika kwa mizani huku wakitoa elimu na mbinu mbalimbali za kubaini vipimo halisi.
Pius alisema kupitia mitandao yao mkoani Manyara wamekuwa wakiwaelimisha wakulima namna ya kutumia mizani kwenye upimaji wa mazao na kuachana na mtindo wa kutumia magunia na madebe.
“Pia wakulima wameendelea kujifunza mbinu mbalimbali za kutambua mizani zinazowaibia wakulima kwa lengo la kuhakikisha wananufaika na mazao yao pindi wakipima uzito wa mazao yao,” alisema Pius.
Alisema walizungumza na wakala wa vipimo nchini ili kuziwezesha halmashauri kutunga na kupitisha sheria ndogo za kutumia mizani za kupima mazao hasa vijijini.
Mmoja kati ya wakulima wa kijiji cha Galapo, Hamis Ibrahim aliipongeza Mviwata kwa namna wanavyoingilia kati suala zima la matumizi ya vipimo kwa wakulima wa eneo hilo.
Alisema awali ilikuwa vigumu wakulima kutekeleza hilo ila Mviwata walizunguka kwa wakulima mbalimbali na kutoa elimu hadi wakatambua haki zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *