Wajumbe wa Kamati ya hamasa wa timu ya Taifa Zanzibar watangazwa

Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya timu ya taifa ya Zanzibar, Ayoub Mohammed Mahmoud ametangaza wajumbe wa kamati hiyo itakayofanya kazi mbali mbali kufanikisha ushindi wa timu hiyo katika mashindano ya chalenji yanayotarajiwa kuanza Disemba 1 nchini Uganda.

Kamati hiyo yenye wajumbe 19 wakiwemo viongozi wa serikali, viongozi wa kisiasa, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida pia itakuwa na jukumu la kukusanya rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya timu hiyo iliyoingia kambini wiki iliyopita.

Akitangaza kamati hiyo, Ayoub alisema hatua hiyo imefikliwa baada ya kupokea barua ya kuteuliwa katika wadhifa huo na Rais wa shirikisho la soka Zanzibar (ZFF) Seif Kombo Pandu wiki iliyopita na baada ya kukaa na uongozi wa shirikisho hilo na timu ya taifa.

Ayoub alisema katibu wa kamati hiyo atakuwa Mohamed Ali Hilal ambae ni Katibu Mkuu wa ZFF na wajumbe ni Kocha Mkuu wa ‘Zanzibar Heroes’ Hemed Suleiman Ali ‘Morocco’, Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba Hemed Suleiman Abdullah, Rajab Ali Rajab Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ na Idrissa Kitwana Mustafa Mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo Omar Hassan Omar ‘King’, Mbunge wa jimbo la Malindi Ali Saleh ‘Alberto’, Meneja wa ‘Zanzibar Heroes’ Ali Mohammed Ameir na Hassan Mussa ‘Haz T’.

Mwewnyekiti huyo aliwataja wajumbe wengine kuwa ni Bahatisha Awadh Suleiman, Issa Kasim Issa ‘Baharia’, Omar Said Shaaban, Mwakilishi wa jimbo la Kikwajuni Ali Salim Ali ‘Al-Jazira’, Mwakilishi wa jimbo la Chumbuni Miraji Mussa ‘Kwaza’, Mwakilishi wa jimbo la Mpendae Dk. Mohammed Said Dimwa, Lagit Ali Fereji, Salum Hilali Salum ‘Kisoda’ na Hafidh Ali Mohamed.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo Mwenyekiti huyo alisema yanaendelea vyema na kwamba kamati yake itajitahidi kuipatia mahitaji yote muhimu kufanikisha maandalizi yake.

“Lengo la kamati hii ni kuijenga timu na kuibua hamasa ya wananchi kuipenda toka mwanzo ili iweze kushiriki kwa mafanikio makubwa mashindano ya mwaka huu nchini Uganda”, alieleza Ayoub.

Aidha alisema lengo la timu hiyo ni kucheza mechi mbali mbali za kujipima nguvu na timu za mikoa yote ya Zanzibar kabla ya mchujo wa mwisho wa wachezaji ambao wapo kambini kwa sasa.

Aliongeza kuwa baada ya kuundwa kwa kamati hiyo, wanatarajia kuunda kamati ndogo ya itakayojumuisha waandishi wa habari za michezo ambayo itakuwa na jukumu la kuitangaza timu katika hatua zote za mashindano hayo.

“Timu ya taifa ni mali ya wananchi ZFF ni waratibu tuu hivyo swala la kuwapasha habari ni la lazima ili kila mmoja ahamasike na kutoa mchango wake”, alieleza Mwenyekiti huo.

Alisema kuwa ili kufikia hatua hiyo mbinu mbali mbali zitatumika ikiwemo ya kutoa jezi ambazo zitauzwa hivyo aliwataka wananchi kuwa tayari kununua jezi hizo zitakapozinduliwa.

“Lengo la kuuza jezi hizo ni kutoa fursa kwa wananchi kuchangia timu yao sio vyenginevyo na kinachotupa moyo ni kuona kuna watu ambao wanataka kwenda Uganda kwa gharama zao wenyewe wao kwa ajili ya kuipa ‘sapoti’ timu yetu”, alisema Ayoub.

Awali akimtambulisha mwenyekiti huyo, Rais wa ZFF Seif Kombo Pandu alisema wamefikia hatua hiyo ili kuongeza ari na hamasa ya ushoindi kwa wachezaji katika hatua za awali za maandalizi ya mashindano badala ya kusubiri timu kufika katika hatua nzuri.

“Katika mashindano yaliyopita timu ilifanya vizuri lakini kwa mwanzo tunaouona katika mashindano ya mwaka huu tuna imani ya kufanya vyema zaidi jambo la muhimu ni kuungana pamoja kuisaidia kamati na timu yetu”, alieleza Kombo.

Jumla ya wachezaji 40 walitangazwa kuunda kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Zanzibar ambao watachujwa kabla ya kusafiri kwenda nchini Uganda kwa ajili ya mashindano ya chalenji ya wakubwa ambayo katika mashindano yaliyopita ‘Heroes’ ilimaliza mashindano hayo ya pili nyuma ya wenyeji Harambee Stars ya Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *