Wadada Wanaouza miili yao Machimboni Shinyanga wapewa semina.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga,Mhe. Azza Hilal Hamad (CCM) akiongozana na madiwani 11 wanawake wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamekutana na wanawake na mabinti wanaoishi katika kata ya Mwakitolyo ili kuzungumza nao namna ya kukomesha vitendo vya baadhi ya mabinti wenye umri kuanzia miaka 12 na wanawake watu wazima wanaofanya biashara ya kuuza miili yao maarufu ‘Chemsha chemsha’ ambapo wanaume hununua ngono kwa kupanga foleni.

Hatua ya mbunge na madiwani hao kukutana na wanawake na mabinti wa Mwakitolyo leo Jumatatu Novemba 18,2019 inatokana na azimio la kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichofanyika Mwezi Agosti mwaka huu ambapo Mhe. Azza aliomba aongozane na madiwani wanawake kwa ajili ya kwenda kuzungumza na mabinti na akina mama ili kukomesha biashara ya ngono katika kata hiyo.

Akizungumza katika kikao cha ndani na wanawake hao wakiwemo wanaomiliki gesti na nyumba za kupanga kilichofanyika katika kijiji cha Nyaligongo,Mhe. Azza amesema biashara ya ngono ni chafu inadhalilisha utu wa mwanamke lakini pia kuwaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya zinaa hivyo inapaswa kupingwa na kila mtu.

“Ndugu zangu biashara ya ngono ni biashara ya kujidhalilisha naomba wanawake na mabinti wanaofanya biashara hiyo kuachana nayo. Tutafute kazi za kufanya ambazo siyo za kujidhalilisha,kazi yeyote ukiipenda na ukaifanya kwa moyo mmoja ni lazima utafikia malengo yako”,amesema Azza.

“Acheni biashara hii.Wanawake tutambue heshima tuliyopewa na mwenyezi Mungu,mama ndiyo anayejua kila kitu katika nyumba,mama ndiye aliyebeba majukumu makubwa katika familia,kwa hiyo tunatakiwa tuibebe heshima tuliyonayo badala ya kufanya biashara hii chafu ya kujidhalilisha”,alisema mbunge huyo.

Mhe. Azza ametumia fursa hiyo kuwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni ‘gesti’ na wanaopangisha vyumba kutoruhusu watu wanaofanya biashara ya kuuza miili kupanga kwenye vyumba.

Aidha amewashauri kuunda vikundi vya ujasiriamali na kuvisajili ili waweze kupata mikopo inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na kwamba hata kama wana biashara zingine basi wajishughulishe pia na kilimo ili wawe na uhakika wa chakula katika familia zao.

“Nitumie fursa hii kumpongeza mtendaji wa kata ya Mwakitolyo na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kwenda kuwatafuta wanawake na mabinti waliokuwa wanafanya biashara na kuwapa elimu ya kuondokana na biashara hiyo na kuwapatia vyerehani ili waweze kufanya biashara ambayo ni halali,jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa biashara hiyo”,ameongeza Azza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *