Waandishi wa Habari Nchini wametakiwa Kutambua thamani ya kazi zinazofanywa na vyombo Vingine (CREDIT),

Wito umetolewa kwa waandishi wa habari nchini kutambua thamani ya kazi iliyofanywa na vyombo vingine pindi wanapotumia kazi za waandishi  au vyanzo vingine vya  habari kutoa habari katika vyombo vyao.

Wito huo umetolewa leo visiwani Zanzibar na mratibu wa mafunzo ya TEHAMA kutoka Shirikia la UNESCO Getruda John,Katika siku ya pili ya mafunzo ya hayo kwa waandishi wa habari wa radio 25 za kijamii.

Bi Getruda amesema kuwa Utandawazi umeifanya Dunia kuwa kijiji hivyo kuwa rahisi kwa waandishi wa habari kutumia habari za watu wengine katika vyombo vyao pasipo kutambua thamani ya vyombo ambavyo vimeibua habari hizo.

Ameongeza kuwa katika miiko ya uandishi wa habari si vyema kwa chombo kutumia habari za chombo kingine bila ridhaa ya chombo kilichotafuta habari hiyo na kwamba kufanya hivyo kunaweza kukufanya ushtakiwe na hata kulipa faini.

Licha ya kusifia kazi nzuri ya kupasha habari inayofanywa na waandishi wa habari za mitandao hasa Blog  Bi Getruda Amewataka wafuate miiko na maadili ya uandishi wa habari hasa katika kutambua mchango wa vyanzo wanapopata habari hizo.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Tehama kutoka UNESCO Ajuaye Mdegela amesema kuwa kitendo cha kutoa thamani ya kazi iliyofanywa na chombo kingine inaonyesha ni jinsi gani umekomaa kitaaluma na unafuata misingi ya uandishi wa habari.

Nao waandishi wa habari wanaohudhuria mafunzo hao wamesema kuwa wengi walikuwa wanajua taratibu za kutoa thamani ya kazi iliyofanywa na chombo kingine ila walikuwa hawana uelewa kuwa unaweza kushtakiwa na kutozwa faini.

Mafunzo hayo ya TEHAMA yanayotolewa na Shirikia la UNESCO yameshirikisha radio 25 za kijamii,Ishirini na moja kutoka Tanzania bara na radio nne kutoka Visiwani Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *