Vyama Vikuu vya Ushirika wa Tumbaku Tanzania (TCJE) Waja na mkakati wa kujenga kiwanda cha kusindika Tumbaku.

DODOMA

SERIKALI imevipongeza vyama vikuu vya Ushirika wa zao la Tumbaku nchini (TCJE) kwa kufikia uamuzi wa pamoja wa kuazimia kuanzisha kiwanda cha kusindika na kuchakata tumbaku ili kuongeza thamani ya zao hilo na hatimaye kupata bidhaa za viwandani zitokanazo na tumbaku.

Pongezi hizo zimetolewa jana Mjini Dodoma na Kaimu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege.

Dr Ndiege amesema kuwa uamuzi wa kujenga Kiwanda hicho utasaidia wakulima kuwa na uhakika wa tumbaku yao kununuliwa ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa wanunuzi wa tumbaku nchini.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Ushirika wa Vyama vya Tumbaku nchini  Bw. Emmanuel Charahani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Tumbaku Wilaya ya Kahama (KACU), amesema kuwa Umoja huo unaundwa na Vyama Vikuu vya Ushirika wa Tumbaku kutoka Kahama (KACU), Katavi (LATCU), Chunya (CHUTCU), Kigoma (KTCU), Tabora (WETCU) na Urambo (Mirambo).

Charahani ameongea kuwa  wazo la kuanzisha kiwanda lilitokana na hali halisi ya Soko la Tumbaku nchini ambapo amesema kuwa kuanzia mwaka  2011 hadi 2013 mahitaji ya wanunuzi yalikuwa wastani wa uzito wa tani 120 wakati changamoto kubwa ikiwa ni kupungua kwa mahitaji na manunuzi ya zao la Tumbaku tani 141 hivi sasa.

Kuhusu bei ya Tumbaku Charahani amesema kuwa imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka akitolea mfano kuwa mwaka 2016/17 bei ya soko ilikuwa ni Dola 2.00, mwaka 2017/18 Dola 1.75, mwaka 2018/19 Dola 1.72. na kwamba  kushuka kwa bei hizo kunaathiri mapato ya wakulima na pato la Taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Titus Kamani amewahimiza  viongozi hao kuendelea kufuatilia kwa karibu taratibu za kuanzisha kiwanda ili Sekta ya Ushirika kupitia Vyama vya Ushirika viweze kushiriki kikamilifu katika kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano chenye dhamira ya kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya Uchumi wa kati kupitia  Uchumi wa Viwanda.

Tume ya Maendeleo ya Ushirika imekutana na viongozi wa Umoja huo (TCJE) kwa lengo la kujadili na kupanga mikakati ya kuendeleza pendekezo la kuanzisha kiwanda cha kusindika Tumbaku ili kuongeza soko la zao hilo  kwa kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *