UN: Somalia imekumbwa na majanga ya COVID-19, mafuriko na uvamizi wa nzige

Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Kibinadamu (OCHA) limetangaza kuwa Somalia inakabiliwa na majanga yaliyosababshwa na mafuriko, uvamizi wa nzige wa jangwani na ugonjwa wa COVID-19.

OCHA imesema Somalia ambayo imegubikwa na miongo mitatu ya vita imeweza kupiga hatua kubwa kisiasa na kiusalama lakini mafanikio hayo yako hatarini kutokana na majanga hayo matatu yaliyoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kwa mujibu wa OCHA takribani watu 500,000 wamefurushwa kwenye maeneo yao kutokana na mafuriko hayo ambayo yameathiri jumla ya watu zaidi ya milioni moja na kusambaratisha biashara, mazao, masoko, na kuwaacha wengi wakipoteza kila kitu, kushindwa kumudu gharama za chakula na kukosa kipato.

OCHA imesema kana kwamba vita na mafuriko havitoshi hujuma ya nzige wa jangwani nayo inawazonga Wasomali ambapo wakulima wengi wamepoteza mazao yao yote.

Na sasa janga la COVID-19 limezusha taharuki nyingine mpya huku mkuu wa OCHA nchini Somalia Justin Brady akionya kwamba mfumo wa Somalia ni dhaifu kuweza kukabiliana na majanga yote haya kwa pamoja ukilinganisha na mataifa jirani, hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa wa kurudisha nyuma hatua zote zilizopigwa kisiasa na kiusalama kwa miongo kadhaa iliyopita na kuiweka tena jamii njia panda.

Kwa sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) linafanyakazi kwa karibu na OCHA na serikali ya Somalia kudhibiti maambukizi ya COVID-19. Somalia ina wagonjwa zaidi ya 2,080 wa corona na vifo karibu 80.

Umoja wa Mataifa na serikali ya Mogadishu wanahitaji dola milioni 57 kwa ajili ya operesheni za kibinadamu na kukabilana na majanga hayo matatu nchini Somalia, lakini hadi sasa fedha zilizopatikana ni asilimia 20 pekee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *