Ubaguzi wa madhehebu ya Kiislamu wapigwa Marufuku Bukoli Geita,Waumini watakiwa kuwa na umoja.

GEITA

Madhehebu ya dini  ya Kiislamu katika kata ya Bukoli mkoani Geita yametakiwa kutokubaguana na kutengana badala yake wawe kitu kimoja katika kuimarisha uislamu na kudumisha umoja katika jamii.

Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Katibu wa Masjid Al-wahab Shehe Ahmed Al-noobiy wakati wa uzinduzi wa Masjid  Al Falaahi uliofanyika katika kata ya Bukoli mkoani Geita.

Al-noobiy amewataka waislamu wa Bukoli kuwa kitu kimoja na kupendana ili kuupeleka uislamu mbele na kuacha tabia ya kujitambulisha kwa dhehebu kwani kitendo hicho kimepelekea maeneo mengi uislamu kukosa nguvu.

Sambamba na hayo Shehe Al-noobiy ameitaka jamii kuondokana na mawazo potofu  kuwa misaada ya misikiti inayojengwa na Jumuiya ya kiislamu ya Isiqaama ya nchini oman inakuwa ya taasisi hiyo na siyo mali ya waislamu wa eneo husika.

Naye mwenyekiti wa Masjid Al-wahab ya Mjini Kahama Mohamed Al-habsy amewataka waislamu kuzitunza nyumba za ibada huku Imamu wa Masjid Al-falaah ya Bukoli Geita Rashid Salum akitoa shukrani kwa niaba ya waislamu wenzake kwa ujenzi wa msikiti huo.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Bukoli Faraji Rajab amewataka wazazi kuendelea kuwasomesha watoto elimu ya dini na elimu ya duniani ili waje kuwa viongozi wa baadaye na kusimamia kikamilifu nyumba za ibada.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *