Uandikishaji vitambulisho vya NIDA,yafikia asilimia 96,wilayani kahama.

Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imesema imefanikiwa kuandikisha vitambulisho vya taifa (NIDA) kwa asilimia 96 ya lengo lililokusudiwa kuandikishwa wilayani humo.

Akizungumzia hatua hiyo katibu tawala Wilaya ya Kahama Thimos Ndanya amesema watu waliokusudiwa kuandikishwa vitambulisho vya taifa (NIDA) ni 326,760 ambapo mpaka sasa jumla ya wananchi 313,303 wameandikishwa ambao ni sawa na asilimia 96.

Ndanya amesema kuafutia zoezi hilo kufanikiwa kwa kiwango kikubwa wananchi wanapaswa kuendelea kujitokeza kujisajili kwa waliosalia na wasisubiri siku ya mwisho iliyotangazwa na rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya usajili wa laini Januari 20 mwaka huu.

Amesema watu wengi wamekuwa hawajitokezi wakati zoezi likiwa linaendelea na linapoelekea mwisho wananchi wanakuwa wengi kitu ambacho kinapelekea kuwa na uhaba wa vifaa pamoja na watumishi lakini wangekuwa wanajitokeza kila siku hali hiyo ingesaidia hadi kufikia siku ya mwisho watu kuwa wachache.

Ndanya amesema baada ya siku kuongezwa za usajili wa laini za simu kwa kutumia namba za vitambulisho vya taifa wao kama serikali ya Wilaya waliamua kupeleka fomu zinazotakiwa kujazwa katika serikali za mitaa kwa Kata zote 58 za wilaya hiyo ili kuwarahishia wananchi kuchukua fomu na kujaza huko huko.

Kwa upande wao wananchi ambao hawajafanikiwa kujisajili vitambulisho hivyo vya taifa wamesema watumishi wa kusimamia zoezi hilo wanapaswa kuongezwa kwani ni wachache pamoja na vitendea kazi kwani bila hivyo siku ya mwisho ya usajili wa laini za simu itafika bado watu wengi hawajapata namba za taifa.

Mmoja wao Mathias Francis amesema kwa jinsi zoezi linavyokwenda serikali inapaswa kuongeza vitendea kazi pamoja na watumishi kwani wamekuwa wakiamka usiku kwenda kupanga foleni lakini bila mafanikio kitu ambacho siku ya mwisho itafika bado hawajakamilisha na simu zao kufungwa.

Aidha zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama z vidole kwa kutumia namba ya vitambulisho vya taifa litafikia ukomo January 20 mwaka huu ambapo pia uandikishaji wa vitambulisho vya taifa kwa wilaya ya Kahama ulianza mwaka 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *