Trump akosolewa vikali kwa kupendekeza kemikali kutumika kama matibabu

Rais wa Marekani Donald Trump amekosolewa na madaktari baada ya kupendekeza utafiti ufanyike kubaini ikiwa virusi vya corona vinaweza kutibiwa kwa kudunga binadamu sindano za kemikali za kuua vimelea vya virusi na bakteria.

Pia alionekana kupendekeza wagonjwa watibiwe kwa mwanga wa kieletroniki -UV , wazo lililopingwa na daktari wakati wa hotuba yake.

Afisa wake mmoja pia awali alisema kuwa mwangaza wa jua na kemikali za kuua vimelea vinafahamika kuua maambukizi.

Kemikali za kuua vimelea ni sumu na yaweza kuhatarisha maisha ya binadamu endapo itachomwa kwa sindano.

Kemi kali hizo pia zinaweza kuwa hatari kwa matumizi ya nje tu hata kwenye ngozi, macho na mfumo wa kupumua.

Katika mkutano wa kikosi kazi cha kukabiliana na virusi vya corona cha Ikulu ya White House na wanahabari siku ya Alhamisi, afisa aliwasilisha matokeo ya utafiti wa serikali ya Marekani ambayo yalionesha kuwa virusi vya corona vinaonekana kudhoofika hata vinapopigwa na mwangaza wa jua au joto.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa blichi inaweza kuua virusi katika mate na ute wa mfumo wa kupumua katika kipindi cha dakika tano, huku pombe ikiua kwa haraka zaidi.

William Bryan, ambaye ni kaimu mkuu wa Idara ya Sayansi wa usalama wa ndani na teknolojia katika wizara ya mambo ya ndani aliainisha katika mkutano na waandishi wa habari juu ya matokeo ya utafiti huo.

Huku akielezea kuwa utafiti huo unapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari, Bwana Trump alipendekeza utafiti zaidi ufanyike kuhusiana na matumizi ya kemikali zakuua vimelea.

“Kwa hiyo, mfano tukipiga mwili na mionzi ya kielekroniki -au ikiwa tukiupiga mwili na mwanga wa nguvu ,” alisema rais, huku akigeuka kumtazama dokta Deborah Birx, mratibu wa White House wa shughuli za kupambana na virusi vya corona, ” na ninadhani ulisema hilo hali kwamba bado halijachunguzwa lakini mtalifanya jaribio.

” Na halafu nikasema, je mfano uingize mwangaza ndani ya mwili, ambao unaweza kuuingiza kupitia mwili au kwa njia fulani nyingine. Na ninadhani ulisema utapima hilo pia hilo. Inafurahisha ,” aliendelea rais.

“Na halafu ninaona kemikali ya kuua vimelea ikiviua kwa dakika moja.Dakika moja. Na kuna njia tunaweza kufanya kitu kama hicho au kusafisha ?

“Kwa hiyo, itafurahisha kuangalia hilo.”

Huku akijinyooshea kidole kwenye kichwa chake, Bwana Trump aliendelea kusema: “Mimi sio daktari. Lakini niko kama mtu ambaye anayeweza kukufanya ufikirie vizuri na kukuambia je unafahamu nini .”

Madaktari wameonya kuwa wazo la rais linaweza kusababisha matokeo mabaya.

Daktari bingwa wa maradhi ya mfumo wa kupumua Dkt Vin Gupta ameiambia BBC kuwa “dhana hii ya kudunga au kuingiza aina yoyote ya kemikali ya usafi ndani ya mwili ni kutowajibika na ni ya hatari .

“Ni njia ya kawaida ambayo watu huitumia wakati wanapotaka kujiua .”

Kashif Mahmood, daktari katika eneo la Charleston, West Virginia, alituma ujumbe wake wa twitter akisema “Kama daktari wa dawa , ninaweza kupendekeza kudunga sindano ya kemikali za usafi ndani ya mapafu au mionzi ya UV ndani ya mwili kutibu COVID-19.

John Balmes, mtaalamu wa tiba ya mfumo wa kupumua katika Hospitali kuu ya Zuckerberg San Francisco alionya kuwa hata moshi kutoka katika blichi unaweza kusababisha matatizo mabaya ya kiafya.

Aliliambia gazeti la Bloomberg News: “Kuvuta hewa ya kemikali ya chlorine inaweza kuwa ni jambo bay asana kwa mapafu. Njia ya hewa na mapafu havikutengenezwa kupokea kemikali za usafi za kuua vimelea.

Awali Bwana trump aliipigia debe dawa ya malaria ya hydroxycloroquine, akisema inaweza kuwa tiba ya virusi vya corona, ingawa ameacha kuishabikia hivi karibuni.

Wiki hii utafiti kuhusu wagonjwa wa virusi vya corona uliofanywa na hospitali ya serikali ya Marekani inayoendeshwa na wanajeshi wa zamani ulibaini kuwa vifo miongoni mwa wale waliotibiwa na dawa ya hydroxychloroquine vilikua vingi kuliko waliotibiwa kwa uangalizi wa kawaida.

Akizungumzia juu ya kauli za rais Alhamisi, Joe Biden anayetazamiwa kukabiliana nae katika uchaguzi wa urais mwezi Novemba, alituma ujumbe wa twitter : “Mwangaza wa UV ?Kudunga sindano za kemikali ya usafi? Hili ndio wazo, Bwana rais: vipimo zaidi.Sasa. Na vifaa vya kinga kwa ajili ya wataalamu wa matibabu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *