TPA yaanika ‘upigaji’ wa magari mipakani

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), imeeleza jinsi ilivyonusuru gari aina ya Benz iliyokuwa ikimilikiwa na raia wa Congo kupigwa mnada baada ya kubainika dhuluma inayodaiwa kufanywa na watendaji wa bandari hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine za umma.

Hali kama hiyo ilisababisha wateja wengi waliokuwa wanaitumia bandari hiyo kupitisha magari yao kuikimbia na kuikosesha serikali mapato baada ya idadi ya magari yaliyokuwa yapitia nchini kuporomoka.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko, alisema shehena ya magari inayopitia Bandari ya Dar es Salaam iliporomoka kiasi cha kumfanya kwenda kufanya uchunguzi.

Alisema mwaka 2014/15 magari 164,000 yalikuwa yakiingia nchini, mwaka 2015/16 yalishuka hadi 127,335 na mwaka 2016/17 yaliporomoka na kufikia 93,471.

“Mporomoko huo ulikuwa kilio cha kusaga meno, niliondoka kwenda kufanya kampeni za wafanyabiashara wa magari mimi binafsi, nilikwenda Lubumbashi nchini Congo, nilisikitika sana huduma zetu zilikuwa za ovyo sana,” alisema na kuongeza:

“Nilikuta tunapiga mnada magari ya watu, mama mmoja nilimkuta anatokwa na machozi, alinunua benzi lake anataka kulipa kila kitu amekataliwa, watu wetu wameamua gari lipigwe mnada, walihakikisha hatafanikiwa kulitoa ndani ya muda.”

Kakoko alisema, gari hilo, lilikuwa limeingizwa kwenye orodha ya mnada kutokana na mazingira yaliyojengeka kuhakikisha mteja huyo hafanikiwi kulitoa kutokana na gharama kubwa kiasi cha kushindwa kuzimudu.

“Wiki hiyo ilikuwa bahati nilikuwapo eneo la tukio, nililitoa kwenye mnada, lakini ilikuwa ni vita kubwa kidogo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema na kuongeza:

“TPA ilimsamehe yule mama tozo zote kwa sababu ya uzandiki na uhuni tuliomfanyia, akalipa tozo za kawaida, hii imerudisha wafanyabiashara wa magari.”

Pia, alisema alikwenda Jiji la Blantyre nchini Malawi ambako magari yanauzwa kama njugu na vijana wadogo wadogo wa jiji hilo huku fedha ambazo zilipaswa kuingia serikalini zikipotea.

“Pale Blantyre, Malawi nilishangaa wanaouza magari ni vijana wadogo wa miaka 20 hadi 21, tulikaa kwenye mawe tukafanya mkutano, walinieleza matatizo yao, mengi ni ya watendaji wa taasisi za serikali,” alisema na kuongeza:

“Walinieleza matatizo yao makubwa, mengi ni ya ndani ya serikali ikiwamo huduma mbaya, ikiwamo rushwa kwenye mpaka wa Kasumuro, ambao ni Malawi na Tanzania.”

Hapo mpakani, Kakoko alisema, walikuwa wanazuiwa kupita hadi asubuhi, lakini wakijichanga na kutoa rushwa wanaachiwa huku magari yakipotea na bima za kufoji ikiwamo usumbufu wa askari wa usalama barabarani.

“Ukiacha matatizo ya TPA ya watu kuiba vifaa vya magari, sababu nyingine zilifanya tukose biashara kiasi cha kufanya wafanyabiashara wa Zimbabwe kuhamia Bandari ya Msumbiji,”alisema.

Akizungumzia vikwazo vya usafirishaji wa magari barabarani, Kakonko alisema gari ni shehena hivyo haitakiwi kupakia mzigo wala abiria.

Alisema wafanyabiashara wa Uganda walimueleza kuwa dereva mmoja alikamatwa eneo la Tinde, mkoani Shinyanga baada ya bampa la mbele ya gari kukatika na kuamua kulitoa na kuliweka ndani ya gari, kitendo ambacho kilisababisha akamatwe na kuwekwa polisi kwa wiki moja.

“Alikaa polisi kwa wiki moja kuthibitisha kweli bampa ilikuwa ni sehemu ya gari au la, baada ya hapo hakutaka kupitisha magari yake huku, lakini niliongea nao na sasa wamerudi na kupandisha rekodi kutoka magari 93,000 hadi 132,035 kwa mwaka 2017/18 , huku mwaka huu yakiwa magari 159,639,” alifafanua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *