TAKUKURU Mkoa Wa Dodoma Yawakamata Viongozi Watatu Chama Cha Ushirika Matumaini Saccos .

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU]mkoa wa Dodoma inawashikilia watu watatu waliokuwa viongozi wa chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Matumaini[Matumaini SACCOS] Kilichopo kata ya Msanga Wilaya ya Chamwino kwa kosa la matumizi mabaya ya Mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 Marejeo ya 2018.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Nov.19,2019 Ofisini kwake,Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.Sosthenes Kibwengo amewataja ,Watuhumiwa hao kuwa ni Bw.Charles Yohana Chilongani mwenye Umri wa miaka 51 ambaye alikuwa meneja ,Bw.Isaya Noah Chigalila [54]ambaye alikuwa Mhasibu na Bi.Mwanahamis Moshi Kaisi [33] ambaye alikuwa karani wa SACCOS hiyo ,wote wakazi wa kata ya Msanga Chamwino .

Bw.Kibwengo amesema uchunguzi wa TAKUKURU Umeonesha kuwa kati ya Mwaka 2011 na 2013 kwa pamoja walichakata bila kupata idhini ya Mrajisi wa vyama vya Ushirika na kuwezesha SACCOS hiyo kupata bila kustahili mkopo wa Tsh.Milioni mia moja arobaini na nane[148,000,000/=] kutoka benki ya Uwekezaji Tanzania [TIB] Kinyume na Matakwa ya Sheria ya vyama vya Ushirika Na.20 ya Mwaka 2003 na kanuni zake za Mwaka 2004.

Katika hatua nyingine Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU Kwa Kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa Mkoa wa Dodoma leo Nov.19,2019 itamfikisha Mahakamani Bw.Ibrahim Hassan Kahogo mwenye umri wa Miaka arobaini na tatu[43] mkazi wa Area A jijini Dodoma kwa Makosa ya Kughushi ,kujifanya mtu Mwingine ,kutoa taarifa za Uongo yote yakiwa ni kinyume cha sharia ya kanuni za Adhabu Sura ya 16 marejeo ya Mwaka 2002.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema Ofisi yake ilipokea taarifa Mwezi Juni 2019 kwamba Mtuhumiwa akiwa katika ofisi za Kamishina wa Kazi jijini Dodoma alitumia njia za Udanganyifu ili kumwezesha kuomba na kuchukua vibali vya kufanya kazi[working Permits]kwa wageni ambao wameajiriwa na Taasisi ya One Acre Fund ya Mjini Iringa.

“Uchunguzi wetu umethibitisha kwamba Mtuhumiwa alighushi nyaraka mbalimbali zikiwemo barua na vitambulisho na kujifanya ni mwajiriwa wa kampuni hiyo na kwamba ana ridhaa yao ya kufuatilia vibali hivyo kwa ajili ya waajiriwa wa kigeni,jambo ambalo sio kweli.Uchunguzi umebaini pia kwamba ,mtuhumiwa amekuwa mara kwa mara akitumia vitambulisho vyenye picha yake na majina ya watumishi wa Taasisi hiyo kudanganya na kumwezesha kupata huduma katika ofisi ya Kamishina wa Kazi”amesema Bw.Kibwengo.

Pia Bw.Kibwengo amesema Mahakama ya Wilaya Ya Kondoa jana Nov.17,2019 ,imetoa hukumu ya shauri la jinai Na.101/2019 na kuwatia hatiani washtakiwa wawili ambao ni Bw.Shaban Maulid Simpi aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Soera na Bw.Abdi Ramadhani Tutupa ambaye ni diwani wa kata ya Soera wilaya ya Kondoa katika makosa ya matumizi mabaya ya Mamlaka na Ubadhilifu kinyume na Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya 2018.

Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU iliwafikisha Washtakiwa hao mahakamani hapo Mwezi Machi,2019 na kuwafungulia mashtaka matatu baada ya uchunguzi wa Ofisi ya TAKUKURU kuonesha kuwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kuingia mkataba na kampuni ya China Railway Seventh Group iliyokuwa ikitengeneza barabara ya Kondoa-Bonga kwa ajili ya kupata eneo la kuchimba mawe pasipo kushirikisha serikali ya Kijiji,na baadaye kufanya ubadhilifu wa Tsh.Milioni moja ,laki tisa na sabini na nne elfu[1,974,000/=] walizopokea kutoka kampuni hiyo.

Mkuu huyo wa TAKUKURU ameendelea kufafanua kuwa,Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kondoa Mhe.Masao amemtia hatiani Mshitakiwa Simpi katika Makosa yote matatu na kumhukumu kifungo cha Miaka mitatu jela kwa makosa yote au kulipa faini ya Tsh.Laki tisa[900,000/=] huku akitakiwa kulipa Tsh.1,974,000/=alizofuja.

Bw.Tutupa alishtakiwa katika Makosa mawili na ametiwa hatiani kwenye kosa moja na kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Tsh.laki tatu[300,000/=]

Sanjari na hayo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.Sosthenes Kibwengo amesema TAKUKURU inaendelea kuwaasa wananchi kuwa,rushwa ni adui wa Haki na Maendeleo hivyo waendelee kushiriki kwa vitendo kuikataa na kuikemea.

Aidha,Bw.Kibwengo ameitaka jamii kutumia Fursa ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wanaoichukia rushwa kwa Matendo yao ili wawe chachu ya Maendeleo .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *