TAKUKURU Dodoma Yamkamata Mwanaume Mmoja Kwa Kujiita Afisa Wa Takukuru Chamwino Ikulu Huku Ikiokoa Milioni 194 Kutoka Kwa Wanachama Wa Saccos.

Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa [TAKUKURU] Mkoa wa Dodoma inamshikilia Bw.Simon Mapunda Jumbe[43]mkazi wa Kisasa jijini Dodoma anayejishughulisha na kazi za ufundi ujenzi ,kwa kosa la kujifanya afisa wa TAKUKURU kinyume na kifungu cha 36 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya mwaka 2018.

Akizungumza na waandishi wa Habari ,Mei 7,2020,mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.Sosthenes Kibwengo amesema katikati ya mwezi April,mwaka huu walipokea taarifa ya mtuhumiwa Bw.Jumbe kuwa anajiita Afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma ambapo amekuwa akiwalaghai watu na kuwadai fedha akisingizia kuwa atawasaidia kuwapatia ajira ndani ya TAKUKURU na Ofisi zingine za serikali.

“Ufuatiliaji wetu umeonesha kuwa mtuhumiwa alimwahidi kaka mtoa taarifa wetu kazi ya udereva ndani ya TAKUKURU na baada ya mtu huyo kumweleza kwamba hana leseni ya udereva daraja C ndipo mtuhumiwa akataka apewe shilingi laki tatu na nusu[350,000/=]ili amsaidie kupata leseni .Baada ya kupata taarifa hii na sisi tukaweka mtego wa kumnasa mtuhumiwa akiwa eneo la Kisasa jijini Dodoma tarehe 14/4/2020”amesema Bw.Kibwengo.

Mkuu huo wa TAKUKURU ameendelea kufafanua kuwa ,awali mtuhumiwa alimweleza mtoa taarifa kuwa TAKUKURU imetangaza nafasi za kazi nane za ajira ya madereva na kwamba kwa kuwa nafasi nne zimeshachukuliwa ,yeye atamsaidia mdogo wake kupata nafasi moja katika zile nafasi zilizosalia.

“Baada ya hapo tuliendelea na uchunguzi na kubaini kwamba mtuhumiwa alishawahi kujiita afisa wa TAKUKURU Chamwino IKULU na kumtapeli rafiki wake wa kike ambaye alimtumia Shilingi laki mbili na elfu kumi na nne[214,000/=]ili amsaidie dada yake amsaidie dada yake kupata ajira serikalini na fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya mafaili na sare za kazi.

Ufuatiliaji zaidi ukatuwezesha kumbaini pia kijana mwingine ,mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma[UDOM] ambaye yeye na baba yake wametapeliwa na Bw.Jumbe ambaye alijiita afisa wa TAKUKURU Chamwino Ikulu jumla ya Tsh.Milioni mbili laki nne na hamsini na mbili elfu na mia tano [2,452,500/=]fedha hizo zilitolewa ili awasaidie kumwezesha mwanafunzi huyo kupata ajira kama msaidizi wa mkurugenzi wa TAKUKURU .

Mtuhumiwa alidai kupatiwa fedha hizo alizokuwa analipwa kidogokidogo na kwamba zilikuwa kwa ajili ya gharama mbalimbali zikiwemo kufungua akaunti ya kupokelea mshahara,sare za kazi,silaha na mafunzo ya kuitumia ,matumizi wakati wa mafunzo,ukarabati wa nyumba atakayoishi akianza kazi,tiketi ya ndege ya wazazi wake kwenda DSM Kushuhudia akiapishwa na kuja Dodoma kutoka DSM na TAKUKURU Mkoa wa Dodoma tunaendelea nauchunguzi.”Amesema.

Wakati huohuo Bw.Kibwengo amesema TAKUKURU mkoa wa Dodoma imewafikisha katika mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kuwafungulia shauri la jinai Na.80/2020 watu watatu ambao ni Bw.Chizenga Masagasi Chimya [56] ambaye ni afisa mtendaji wa kijiji cha Muungano wilaya ya Chamwino na Wistone Chagulula[45] mwenyekiti wa kijiji hicho kwa makosa kuomba na kupokea hongo ya Tsh.elfu sabini[70,000/=]ili waweze kuhamisha lalamiko la mtoa taarifa kwenda polisi kwa hatua zaidi.

Wa tatu ni Bw.Ivani Nganje [48]ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Iyoyo kilichopo katika kijiji cha Muungano wilayani Chamwino naye alifikishwa mahakamani kwa kosa la kushawishi na kupokea Tsh. Elfu ishirini na tano [25,000/=]kutoka kwa mtoa taarifa huyo ili aitishe baraza la kitongoji kwa lengo la kusikiliza lalamiko lake makosa hayo yote ikiwa ni kinyume na kifungu cha 15[1][a] cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa,sura ya 329 marejeo ya 2018.

Aidha,Bw.Kibwengo amebainisha kuwa katika kuendelea kutekeleza agizo la serikali la kufuatilia madeni ya vyama vya ushirika ,kwa kipindi cha April,2020 TAKUKURU mkoa wa Dodoma imefanikiwa kurejesha shilingi Milioni hamsini na saba laki tano sitini na sita elfu mia mbili themanini na mbili na senti hamsini[57,566,232.50/=]kutoka kwa viongozi na wanachama 41 wa vyama sita vya akiba na mkopo[SACCOS]Waliochukua wakidaiwa kwa muda mrefu.

Kutokana na takwimu hizo Bw.Kibwengo amesema hadi sasa TAKUKURU mkoa wa Dodoma imeshaokoa Jumla yaTsh.milioni mia moja tisini na nne na kuanzia wiki ijayo kwa kushirikiana na Mrajis wa Msaidizi wa vyama vya ushirika watakabidhi fedha hizo kwa SACCOS husika zinazostahili.

Pia.Bw.Kibwengo ametumia fursa hiyo kukikumbusha chama cha Walimu Tanzania[CWT] mkoa wa Dodoma ambacho kinaendelea na chaguzi kwa ajili ya kupata viongozi wapya kufanya uchaguzi uhuru na haki bila mianya ya rushwa ili kupata viongozi bora na TAKUKURU inaendelea kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *