Taifa Stars kambini kuiwinda Rwanda

KIKOSI cha timu ya Taifa (Taifa Stars), kimeingia kambini jana tayari kuanza maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Rwanda (Amavubi), unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 12, mwaka huu jijini Kigali.

Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda, alisema jana kuwa kikosi hicho kitaanza mazoezi rasmi leo, baada ya wachezaji wote waliopo hapa nchini kuripoti.

Mgunda alisema wamefurahishwa na muitikio wa nyota wote walioitwa katika kikosi hicho, na anaamini watakapoanza mazoezi, wataendelea kuona ushindani wa kuwania namba unaongezeka.

“Timu inaripoti leo (jana), na mazoezi yataanza kesho (leo), hivi sasa tutaamini kila mchezaji anajua jukumu lake, ni mchezo wa kirafiki, lakini ni muhimu sana kwetu,” alisema Mgunda.

Taifa Stars inatarajia kutumia mchezo huo kujiandaa na mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), dhidi ya Sudan utakayochezwa Oktoba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa El Merreikh Omdurman nchini humo baada ya ule wa awali kukubali kipigo cha bao 1-0 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *