KWANDIKWA
USHETU

TAARIFA: MH KWANDIKWA KUAGWA DAR,DODOMA NA SHINYANGA KISHA KUZIKWA USHETU.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias John Kwandikwa anatarajiwa kuagwa katika mikoa mitatu kabla ya kufikishwa kijijini kwake alipozaliwa Butibu Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaamu, Dodoma pamoja na mkoa wa Shinyanga ambapo ibada itafanyika katika kanisa la Katoliki parokia ya Carol Lwanga Kahama kabla ya kwenda kijijini kwake kwenye maziko.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 3, 2021, Katibu wa CCM Emmanuel Mbamange, aliwataka wananchi wa jimbo la Ushetu kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea na maandalizi ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.

Alisema Agosti 6, marehemu Kwandikwa ataagwa jijini Dar es Salaam na baadaye kuelekea nyumbani kwake Kibaha kwa ajili ya kuagwa na majirani zake na Agosti 7 atapelekwa jijini Dodoma kwa ajili ya kuagwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Aidha Mbamange alisema, Agosti 8, mwili wa marehemu Kwandikwa utaagwa Kahama na baadaye kuelekea nyumbani kwake kijiji Butibu na Agosti 9 mazishi yatafanyika Butibu alipozaliwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Festo Kiswaga alisema, marehemu ameacha historia nzuri itakayokumbukwa na wananchi wake kwa kutatua changamoto katika sekta ya afya, elimu, kilimo pamoja na miundombinu ya barabara.

Naye Diwani wa Nyamilango, Robert Mihayo alisema, kwandikwa alikuwa na mipango mikubwa ikiwemo kuongeza maeneo ya utawala katika kuhakikisha siku za usoni wanapata wilaya ambayo itakuwa inajitegemea.

CREDIT:MWANANCHI DIGITAL

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *