Sudan: Jeshi lakabiliana na vikosi vilivyokuwa vitiifu kwa rais aliyepinduliwa Omar al Bashir

Mapambano yalianza Jumanne katika jiji la Khartoum ambapo milio ya milipuko ilisikika na kulazimisha uwanja wa ndege jijini humo kufungwa kwa muda.

Serikali inaadai kuwa uasi huo umechochewa na mlipo ya mafao, kitengo hicho cha usalama wa taifa kwa sasa kinavunjwa.

Wanajeshi wawili waliuawa na wengine wanne kujeruhiwa kwenye uasi huo.

Kiongozi mwandamizi wa baraza huru linaloongoza Sudan kwa sasa, Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, amemtuhumu mkuu wa zamani wa usalama wa taifa Salah Gosh kuchochea uasi huo.

Japo Dagalo anasema hachukulii jambo hilo kama jaribio la mapinduzi, lakini amesema jambo hilo halivumiliki.

Kufikia leo asubuhi jeshi lilikuwa likiyashikilia makao makuu ya kikosi hicho.

Katika hotuba yake leo Jumatano kiongozi wa baraza hilo Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametangaza kuwa mapambano yameisha.

“Makao makuu yote yapo chini ya jeshi, na anga yetu imefunguliwa,” amesema.

Kumekuwa na wasiwasi juu ya uwezekao wa baadhi ya viongozi waliokuwa na ushawishi wakati wa Bashir kujaribu kutatiza mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo kwa hivi sasa.

Bashir ambaye alikaa madarakani kwa mkono wa chuma kwa miaka 30 alipinduliwa mwezi Aprili mwaka jana baada ya kuchacha kwa maandamano ya umma.

Askari kutoka kitengo cha usalama wa taifa walipakia mtandaoni picha za video zikionesha wenzao wakifyatua risasi hewani usiku kama alama ya uasi na kuonesha nguvu zao.

Shirika la habari la Reuters linanukuu raia wakidai kuwa kulikuwa na mapambano ya katika wilaya ya kaskazini Khartoum, na jengo la usalama karibu na uwanja wa ndege kutekwa na waasi.

Vyanzo ndani ya jeshi vinaeleza kuwa vikosi vya serikali kwa sasa vimerejesha hali ya utulivu katika maeneo ambayo waasi walikuwa wakishambulia baada ya kufanya mazungumzo nao.

Kundi kubwa la waandamanaji wa nchi hiyo wametoa wito wa kukomeshwa kwa “oparesheni hizi zisokuwa na msingi ambazo zinawatia hofu wananchi.”

Waandamanai zaidi ya 170 waliuawa mwaka jana nchini Sudan, na kikosi hicho cha usalama wa taifa kipo lawamani kwa kutekeleza sehemu kubwa ya mauaji hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *