Simba yapigia hesabu kushinda mechi zote za Dar

NYOTA namba moja ndani ya Klabu ya Simba Clatous Chama amesema kuwa wachezaji wapo tayari kwa ajili ya ushindani ndani ya ligi na wanahitaji pointi tatu kwenye mechi zote ambazo watacheza ndani ya Ligi Kuu Bara.

Chama akiwa ametumia dakika 270 kwenye ligi ambazo ni mechi tatu alizocheza na zote akiyeyusha dakika 90 amefunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao kati ya saba ambayo yamefungwa na timu yake kwa msimu wa 2020/21.

Kiungo huyo ambaye ni chaguo namba moja la Kocha Mkuu wa Simba kwa sasa, Sven Vandenbroeck amesema kuwa anaamini kazi kubwa ya wachezaji ni kutafuta pointi tatu na hesabu zao ni kuona wanashinda mechi zao zilizopo mbele yao.

“Tunachokiangalia kwa sasa ni kuona namna gani tunaweza kupata matokeo ambayo yatatuwezesha kupaa pointi tatu muhimu kwenye kila mchezo ambao tutacheza ndani ya ligi.

“Naamini tukiweza kushinda mechi zetu za hapa Dar kabla ya kutoka nje tena kwani malengo yetu msimu huu ni kuona kwamba tunaweza kufikia malengo tuliyojiwekea hatutakuwa tayari kuona tunashindwa kuyafikia malengo hayo,” amesema.

Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi tatu ikiwa na pointi saba kibindoni na kinara ni KMC wenye pointi 9.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *