SIMBA KAZI IPO LEO MBELE YA RUVU SHOOTING, TAMBO ZATAWALA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba, leo wana kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting ambayo nayo ni timu ya wajeda kama ilivyokuwa kwa Tanzania Prisons ambao waliwachezesha ligwaride kwa kuwafunga bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela.
Kazi kubwa kwa Simba inayonolewa na Sven Vandenbroeck ni kwenye kusaka rekodi ya kuendeleza ubabe wao mbele ya Ruvu Shooting inayonolewa na Kocha Mkuu, Charles Mkwasa.

Rekodi zinaonyesha kuwa tangu msimu wa 2010/11 timu hizo zimekutana mara 18 ambazo ni dakika 1,620 na Simba imeshinda mechi 16 ambazo ni dakika 1,440 na sare mbili ambazo ni dakika 180.

Jumla ya mabao 51 yamekusanywa ikiwa ni wastani wa kushuhudia bao moja kila baada ya dakika 31 na Simba imefunga mabao 43 huku Ruvu Shooting ikifunga jumla ya mabao nane.

Vandenbroeck amesema kuwa matokeo yao ya mechi iliyopita ambayo walipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons ni sehemu ya matokeo hivyo watapambana kupata pointi tatu kwenye mechi zao za mbele ikiwa ni pamoja na ya leo dhidi ya Ruvu Shooting.

Masua Bwire, Ofisa Habari wa Ruvu Shooting amesema kuwa wataendeleza sera yao ya kung’uta na kupapasa bila kuhofia wanakutana na nani uwajani.

Rekodi zaibeba zaidi Simba

Kwenye mechi nane za mwisho za misimu minne nyuma ambazo timu hizi zimekutana Simba imefanikiwa kushinda mechi saba huku Ruvu Shooting ikiambulia sare moja.

Matokeo yalikuwa namna hii:- 2016/17 Simba 2-1 Ruvu Shooting. Ruvu Shooting 0-1 Simba.2017/18 Simba 7-0 Ruvu Shooting, Ruvu Shooting 0-3 Simba.

2018/19,Ruvu Shooting 0-5 Simba, Simba2-0 Ruvu Shooting. 2019/20, Ruvu Shooting 0-3 Simba, Simba 1-1 Ruvu Shooting.

Ubora wa Simba upo hapa

Ubora wa Simba umejificha kwenye safu ya ushambuliaji ikiwa imefunga mabao 14 kwenye mechi sita na wameokota mabao matatu nyavuni.

Mkwasa tatizo kwa Simba

Mkwasa, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba msimu uliopita akiwa na kikosi cha Yanga mchezo wa kwanza alifanikiwa kupindua meza kibabe kwenye sare ya mabao 2-2, na raundi ya pili akiwa kocha msaidizi wa kikosi hicho Yanga ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Tatizo la Ruvu

Ruvu Shooting kumekuwa na ugumu kwenye safu yao ya ushambuliaji ambapo hadi sasa kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao matatu kwenye mechi saba huku wakiruhusu mabao manne.

Watakaokosekana

Kwa Simba ni Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu, Shomari Kapombe, Gerson Fraga na Ibrahim Ame ambao watakuwa nje ya uwanja kutokana na kuuguza majeraha.

Kwa upande wa Ruvu Shooting kwa mujibu wa Masau Bwire Ofisa Habari ameliambia Spoti Xtra kuwa wapo kamili gado.

Simba ipo nafasi ya nne imeshinda mechi nne na sare moja na kupoteza mechi moja ikiwa na pointi 13 inakutana na Ruvu Shooting ambayo ipo nafasi ya 11 ikiwa imeshinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza mechi mbili na ina pointi tisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *