Simanzi, watoto watatu wa familia moja wafa maji Dar es salaam

Hakuna ajuaye siku wala saa ambayo ataondoka duniani. Kifo kimefanywa kuwa fumbo kubwa la imani.
Baada ya kuondoka nyumbani wakiwa na furaha na kwenda ufukweni kubarizi, hawakujua kama ndugu zao Khalfan Said (17), Jalila Said (15) na Rummani Said (14) watafikwa na umauti.
Watoto hao wa familia moja walikufa kwa kuzama baharini juzi wakiwa kwenye Ufukwe wa Bamba, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Baba mzazi wa watoto hao, Said Saleh Omar akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwake eneo la Tandika Majaribio jijini Dar es Salaam alisema siku ya tukio hilo watoto wake walikwenda ufukweni kuburudika na kujipumzisha jambo ambalo wamekuwa wakilifanya mara kwa mara, lakini juzi walikutwa na umauti.
Akiwazungumzia watoto hao alisema Khalfan alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Istiqama ya Pemba, Jalila alikuwa akisoma Tandika Sekondari na wote walikuwa wakitarajia kuingia kidato cha pili mwakani, huku Rummani akiwa anasoma Shule ya Msingi Tandika na alikuwa anatarajiwa kuingia darasa la saba mwakani.
Alisema pia katika ajali hiyo wamempoteza mtoto mwingine wa ndugu yao waliyemtaja kwa jina la Mariam Ramadhani mwenye umri wa miaka 14.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *