Shule iliyochangiwa milioni 5 na Rais Magufuli yakumbwa na uhaba wa walimu Kahama

Shule ya msingi Mayila iliyopo mtaa wa Mayila Kata ya Nyihogo katika halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga inakabiliwa na uhaba wa walimu baada ya kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 360 na wanafunzi wa darasa la awali 140.

Shule hiyo ni mpya ambayo imejengwa mwaka jana ambayo pia ilichangiwa fedha na rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli na mwaka huu imefunguliwa kwa kuanza kuandikisha wanafunzi shuleni hapo.

Uhaba huo umeibuliwa katika baraza la madiwani wa halmashauri hiyo katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika jana ambapo diwani wa Kata ya Nyihogo Shadrack Mgwami amesema shule ya Mayila mpaka sasa ina walimu watatu ambao hawakidhi mahitaji ya ufundishaji hivyo halmashauri inapaswa kuongeza walimu.

Mgwami amesema hadi sasa zoezi la uandikishaji wanafunzi bado unaendelea lakini walimu waliopo hawatoshi kwani katika mgawanyo wa kila darasa wanafunzi 45 shule hiyo inapaswa kuwa na walimu wapatao 14 ikiwa kwa sasa wapo watatu hivyo wanatakiwa kuongezwa walimu 11 ili kukidhi mahitaji ya shule.

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba amesema changamoto hiyo ipo lakini kwa sasa hana uwezo wa kuongeza walimu kutokana na serikali bado haijatangaza kuajiri walimu hivyo ajira za walimu zikitoka atapeleka walimu shuleni hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *