Shambulio la Al-shabab lilivyoathiri usalama eneo la Lamu

Jeshi la jeshi la Kenya, KDF limethibitisha wanajeshi watatu wa Marekani na wajenzi wawili wa ulinzi wameuawa katika shambulio la siku ya Jumapili katika eneo la Manda bay.

Jeshi la Kenya limethibitisha vifo hivyo na kusema kuwa Wamarekani wengine wawili wafanyikazi wa kitengo cha ulinzi katika jeshi la Marekani walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea karibu na mpaka wa Somalia.

Jeshi hilo pia limeelezea kuwa wanamgambo wanne wa Al-shabab waliuawa katika kambi ya Simba iliyoko eneo la Hindi Magogoni pembezoni mwa kisiwa hicho cha kitalii Lamu.

Marekani kwa upande wao wamepuuza shambulio hilo na kudai lilidhibitiwa vilivyo.

Ndege nne za kijeshi mbili za Kenya na zingine mbili za Marekani ziliaharibiwa vibaya katika tukio hilo.

Hali hiyo iliwatia hofu wakaazi wa kisiwa cha Lamu, mmoja wao akiwa mama ambaye hakutaka kutajwa jina kutokana na sababu za kiusala aliiambia BBC:

”Nilisikia sauti ya risasi ni kamuamsha bwanangu… na ndio sasa marisasi yalikuwa yanazidi, ikabidi ni toke niingie mvungu mwa kitanda manake risasi zilikuwa zinalia juu ya paa la nyumba, nikaenda chumba cha watoto cha kulala nikawapta watoto wanalia na ndipo baba yao akanza kuwatuliza”

Anasema ”Risasi ziliendelea kulia hivyo hivyo sasa hakuna kutoka, hakuna kuenda mahali popote kwa nyumba juu unaona moto tu”.

Shambulio hilo la kambi ya kijeshi limetokea siku tatu baada ya shambulizi lengine lililolenga mabasi ya matatu ya abiria yaliyokuwa yamebeba abiria kutoka Mombasa kuelekea Lamu siku ya Alhamisi ambapo watu wanne walipoteza maisha yao.

Wakati vyombo vya usalama nchini Kenya vikiendelea kudhibiti hali na kutoa usalama kwa wananch wakaazi wa eneo hilo la Lamu wanahofia hali yao ya usalama hasa kufuatia kuripotiwa kwa mashambulizi mawili ya kigaidi

”Haya matatizo ambayo yametokea kuanzia juzi magari kupigwa na jana maeno karibu na uwanja wa ndege kushambuliwa wakati huu ambao shule zinafunguliwa inatutua hofu” alisema Misbaa Aboubakar ambaye ni mkaazi na mzazi ambaye mtoto wake anafaa kurejea shuleni.

”Twataka tuwapeleke shule…Hatujaelewa mpapa saa hii wametupangia nini juzi baada ya masuala ya juzi kupigwa gari na jana kupigwa uwanja wa ndege” alisema Bwana Aboubakar.

Anataka serikali iwabainishie wakaazi wa Lamu mkakati wa kiusalama ili kuwaondolea hofu kuhusu masuala ya usafiri” alisema Bw. Aboubakar.

Wakati ambapo hali ya usalama ikiendelea kukumbwa na changamoto katika eneo hilo huenda sekta ya utalii ambayo ni kitega uchumi wa Lamu ukaathirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *