Baadhi ya wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia kitendo cha kuharibika kwa mashine ya vipimo vya Mionzi (digital, X- ray) na kusababisha kutofanya kazi katika hospitali ya halmashauri ya Mji wa Kahama.
Malalamiko hayo yametolewa jana (Dec 19) katika kundi la Mtandao wa Whatsap la Kahama News ambapo baadhi ya wateja wameonekana wakilalamikia kuhusu kukosekana huduma hiyo.
Katika malalamiko hayo baadhi ya wateja wameshangazwa kuambiwa huduma hiyo haipatikani kwa sasa kutokana na kuharibika kwa mashine hiyo huku wakidai kuwa wamelipia kiasi cha shilingi 5,000 kwaajili ya kupata kadi ya kwenda kuonana na daktari.
Katika mjadala huo uliodumu kwa dakika kadhaa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mji wa Kahama ANDERSON MSUMBA amekiri kuharibika kwa Mashine hiyo na kusema kuwa mashine hiyo ni mpya na ya kidigtali ambapo ipo chini Bohari Kuu ya dawa Tanzania, (MSD).
Amesema tayari wamewasiliana na MSD kwaajili ya kumtuma fundi ambapo alipaswa kufika siku ya juzi na kwamba atafika leo kwaajili ya kulishughulikia hilo ambapo ameomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza na kwamba halmashauri hiyo inampango wa kununua Mashine ya X RAY katika kituo cha afya Mwendakulima.
Kuhusu malipo ya Shilingi 5,000 MSUMBA amesema kwamba shilingi 3,000 ni kwaajili ya kadi, na shilingi 2,000 ni kumuona daktari na kwamba bila ya kumuona daktari huwezi kujua vipimo vya kufanya huku akiwataka wananchi kujiunga na Mfuko wa bima ya afya ya CHF iliyoboreeshwa.