Serikali Kuendelea Kuboresha Idara Ya Uthibiti Ubora Wa Shule Kwa Lengo La Kupata Wahitimu Bora

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali itaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa elimu kwa kuboresha Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kwa lengo la kuhakikisha Elimu inatolewa kwa kiwango ili kupata matokeo na wahitimu bora.
Profesa Ndalichako amesema hayo ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma alipokuwa akitoa tathmini ya matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na nne ambapo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha inazifikia shule na kuwa karibu nao zaidi na tayari wathibiti ubora 400 wameajiriwa.
“Katika kuimarisha uthibiti ubora wa shule mwaka huu tumeajiri wathibiti ubora 400 ili kuimarisha utendaji wa idara hii na kuwafikia wadau na shule ili kuziwezesha kuboresha ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Profesa Ndalichako.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema matokeo haya ni ya kwanza tangu kuanza kutekeleza Mpango wa Elimu bila Malipo ambao baadhi ya watanzania hawakuamini kama ungefanikiwa lakini matokeo yameonyesha mafanikio na ufaulu umeongezeka kutoka 67.91% mwaka 2015 hadi kufikia 80.65% mwaka 2019.
Wakati huo huo Ndalichako kwa niaba ya Wizara amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani yao pamoja na walimu kwa kuwa bega kwa bega na wanafunzi wao na kuwawezesha kupata matokeo mazuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *