Buhari atoa wito amani huku jopo likianza uchunguzi wake

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametoa wito wa kudumishwa kwa amani huku jopo likianza kuchunguza unyanyasaji unaotekelezwa na polisi hii leo Jumatatu, uliotokea katika mji wa kibiashara wa Lagos.

Jopo hilo la uchunguzi ni miongoni mwa mahitaji ya waandamanaji wanaotaka maafisa wa polisi watakaopatikana na makosa ya unyanyasaji wachukuliwe hatua kisheria.

Pia wanataka waathirika wa ukatili unaotekelezwa na polisi au jamaa zao kufidiwa na serikali.

Mji wa Lagos ulikuwa wa kwanza miongoni mwa majimbo 36 kuanzisha jopo hilo na pia limetaka raia kuwasilisha malalamishi yao.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter, Rais Buhari alisema anaunga mkono kikamilifu jopo hilo.

Alisema amekuwa akijiepusha kuingia kwenye mjadala wa mauaji yaliyotokea kwenye lango la Lekki, hadi ushahidi wote utakapokusanywa, kulingana na taarifa kutoka kwa ofisi yake.

“Rais alishauri kwamba amani, undugu, na masikizano miongoni mwa jamii ni ya msingi katika maadili yao na kusihi raia wa Nigeria kutogeukiana kwa chuki’,” taarifa iliyotolewa imesema.

Uchunguzi unaanza ikiwa ni karibu wiki mbili za maandamano kote Nigeria yaliyotekelezwa na vijana wanaotaka mabadiliko katika idara ya polisi na vile nchi hiyo inavyoendeshwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *