Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani Colin Powell amekuwa Mrepublican wa kwanza mashuhuri kutangaza wazi kumuunga mkono mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden katika uchaguzi wa rais Novemba mwaka huu.
Powell ameiambia televisheni ya CNN kuwa Rais Donald Trump amejitenga na katiba ya Marekani na ni kitisho kwa demokrasia ya nchi. Powell, ambaye ni jenerali mstaafu wa jeshi, pia amewashutumu viongozi wenzake wa Republican kwa kushindwa kumdhibiti Trump na kumuwajibisha.
Hivyo ametangaza kuwa atampigia kura mpinzani wa Trump, ambaye ni makamu wa rais wa zamani Joe Biden. Biden amemshukuru Powell kwa kumuidhinisha, akiandika kwenye Twitter kuwa hili sio suala la siasa, bali ni kuhusu mustakabali wa nchi.