Ninaendelea vizuri namshukuru mungu kwa kutuponya- Zitto Kabwe

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-wazalendo, Zitto Kabwe aliyehusika katika ajali ya barabarani siku ya Jumanne akiwa na wenzake wanne amesema anaendelea kupata nafuu.
Kupitia ujumbe alioandika kwenye mtandao wake wa Twitter Bw. Zitto alisema: ”Ninaendelea vizuri. Ilikuwa ajali mbaya sana. Namshukuru Allah kwa kutuponya. Shukran Wahudumu wa Kituo cha Afya Kalya, licha ya changamoto, Huduma ya kwanza imetusaidia. Shukran Madaktari na Wahudumu Hospitali ya Maweni Kigoma. Mimi na wenzangu, mpaka sasa, ni wazima.”

Kiongozi huyo na wenzake wanne walipata ajali, jimboni Kigoma Kusini, Magharibi mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa bara, Joran Bashange, ajali hiyo ilitokea akiwa kwenye shughuli za kampeni, akitoka katika eneo la kata ya Kalya kuelekea Lukoma.

”Gari lake liligongwa nyuma kisha likapoteza mwelekeo na kupinduka zaidi ya mara mbili.”

Imeelezwa kuwa gari lake lilikuwa na abiria watano ambao wote wako salama, lakini wamepata maumivu na majeraha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *