Mzee wa miaka 70 ashambuliwa na Fisi akiwa amelala usiku Kahama.

Mkazi wa kijiji cha chela katika Halmashauri ya Msalala Mkoani Shinyanga, Buluba Jilasa (70) amejeruhiwa na fisi kwa kung’atwa sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa amelala.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Halamashauri ya Mji wa kahama Jilasa amesema tukio hilo limetokea jana usiku wakati akiwa amelala, nyumbani kwake alishituka mlango ukivunjwa na fisi huyo ambaye aliingia hadi chumbani na kuanza kumjeruhi.

“Nimepambana naye ili asimdhuru,lakini alifanikiwa kuning’ata kiganja cha mkono wa kushoto na kunisababishia majeraha makubwa katika maeneo mbalimbali ya mwili wangu”alisema Jilasa.

Amesema aliweza kumdhibiti fisi huyo  ambaye baadae alianza kushambulia kuku na ndipo alipotoka na kwenda kumgongea mjukuu wake Charles Bushemeli kwaajili ya kuomba msaada.

Nae afisa Mtendaji wa kijiji cha Chela Zaphline Samweli amesema tukio la fisi kuvamia kwenye mkazi ya wananchi sio lakwanza na wamekuwa wakivamia nyakati za usiku na kushambulia mifugo kama vile Ng’ombe, Mbuzi pamoja na Punda kutokana na uwepo wa milima mingi.

Amesema  mapango yaliyopo kwenye milima iliyopo kijijini hapo ndio makazi ya wanyama hao  wanapojificha na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kwa maafisa maliasili pindi wanapowaona wanayama hao.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya mji wa kahama Dk George Masasi amethibitisha kumpokea  majeruhi huyo ambaye alikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na ameshaapatiwa huduma ya  matibabu na anaendelea vizuri.

“Tumemchoma sindano ya  kuzuia asipate kichaa kinachotakana na kung’atwa na fisi(Anti Rabies)na  mkono wake wa kushoto umeshambuliwa vibaya unatakiwa kukatwa kiganja alisema Masasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *