MWAKINYO KUTETEA UBINGWA WA WBF DHIDI YA MUARGENTINA

BONDIA mzawa, Hassan Mwakinyo amebadili ratiba ya mazoezi na sasa anajifua masaa manne kwa siku ikiwa ni maandalizi ya pambano lake dhidi ya Muargentina Jose Carlso Paz.
Mwakinyo ameweka kambi eneo la Magoroto, Muheza mkoani Tanga kuelekea pambano la kutetea ubingwa wa mabara wa WBF na kuwania ubingwa mpya wa mabara wa IBA wa uzito wa super-welter.

Bondia huyo anajifua chini ya kocha, Hamis Mwakinyo pamoja na wasaidizi mbalimbali huku wakitumia video mbalimbali kumsoma Paz ambaye ana rekodi nzuri.

“Nimehama nyumbani na kujichimbia huku Magoroto kwa lengo la kufanya vyema katika pambano hilo, ninajifua zaidi ya raundi 12 ili kupata stamina ya kwenda sambamba na mpinzani wangu,” amesema Mwakinyo.

Katika hatua nyingine, waandaaji wa pambano hilo wamesema kuwa tiketi kwa ajili ya pambano hilo zitauzwa mtandaoni kupitia kampuni za Nilipe na Selcom.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema kuwa viingilio kwa pambano hilo vitaanzia Sh 150,000 kwa eneo la kawaida na meza ya watu 10 itauzwa kwa sh milioni 3 ambao watapata huduma mbalimbali zilizoandaliwa.

Twissa amesema kuwa mbali ya Mwakinyo na Paz, pia siku hiyo kutakuwa na mapambano makali ambapo bondia nyota wa kike, Zulfa Macho atazipiga na Alice Mbewe kutoka Zambia wakati Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu katika uzito wa super-middle.

Siku iyo pia bondia nyota kutoka Kenya, Fatuma Zarika atazichapa na Patience Mastara wa Zimbabwe katika uzito wa super bantam.

Wakati huo huo; mpinzani wa Mwakinyo, Paz ameamua kuwasili mapema Tanzania ili kuzoea hali ya hewa.

Paz anatarajiwa kuwasili usiku kwa ndege ya KLM na msafara wake utaambatana na kocha wake, Oscar Alberto Ramon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *