Mvua zinazoendelea kunyesha zaacha watu 1,000 bila makazi Dodoma

Zaidi ya watu 1,000 wamekosa makazi, baada ya nyumba 237 kubomolewa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Dodoma.

Wakazi walioathirika kutokana na mvua hizo ni wa Wilaya ya Bahi, huku miundombinu ya barabara ikiharibiwa.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mwanahamisi Munkunda, alipokuwa akizungumza jana, baada ya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.

Katika ziara hiyo, Munkunda aliambatana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na madiwani ili kujionea uharibifu uliojitokeza na namna ya kuwasaidia watu walioathirika.

Munkunda aliyataja maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo ni Bahi Sokoni, Bahi Misheni, Mji Mpya na Nkogwa pamoja na vijiji vya Mbuyuni, Uhelela, Laloi, Mugu na Nagulo.

Nyumba zilizoathirika Mahi Sokoni ni 80, Mzongole 92, Uhelele nyumba 3 na Nagulo Bahi (30).

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, huku akiwataka wazazi kuhakikisha watoto wanacheza kwenye maeneo salama badala ya kuogelea kwenye mito na madimbwi yaliyojaa maji.

Alisema kuna mito mingi ya maji kutoka mikoa jirani na wilaya inayoishia katika Wilaya ya Bahi, hivyo wananchi wachukue tahadhari kutokana na maji kuingia kwenye makazi ya watu.

“Ukiwaacha watoto au mtu mzima akitegemea kuwa maji yaliyopo ni yale ya siku zote, kumbe yameongezeka…tuwe makini ukiona mto umefurika usipite mpaka ujiridhishe maji yamepungua,” alisema.

Hata hivyo, alisema wameomba kiasi cha Sh. milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu yakiwamo madaraja yaliyoharibiki, na kwamba fedha hizo zimeshapelekwa na zitaanza kutengeneza miundombinu hiyo.

“Serikali iko makini kuhakikisha shughuli za kiuchumi hazisimami kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema.

Alibainisha kuwa mito mingi imeacha njia zake za asili, hali inayosababisha hata maji kupita juu ya madaraja na wananchi kushindwa kuvuka kwa kuhofia usalama wao.

Mkuu huyo wa wilaya aliagiza kukarabatiwa kwa daraja la Mto Nkigwa ambalo limeanza kukatika kutokana na mvua hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *