Mtawala wa muda mrefu Oman, Sultan Qaboos amefariki akiwa na umri wa miaka 79

Sultan alimng’oa madarakani baba yake katika mapinduzi ya amani kwa ushriikiano na Uingereza mwaka 1970 na kuiweka Oman katika mwanzo mpya wa maendeleo kwa kutumia utajiri wake wa mafuta.

Alikuwa maarufu sana na mfalme wa nchi hiyo, na yeyote aliyejitokeza kumpinga alinyamazishwa.

Sababu za kifo chake bado hazijathibitishwa.

Ndugu yake Haitham bin Tariq Al Said ameapishwa kama mrithi wake.

Aliyekuwa waziri wa utamaduni na thurathi za kitaifa ameapishwa leo Jumamosi baada ya mkutano wa Baraza la Familia ya Kifalme, serikali imesema.

Sultan ndo mwenye kufanya maamuzi nchini Oman. Pia anashikilia wadhifa wa waziri mkuu, amiri jeshi mkuu, waziri wa ulinzi, waziri wa fedha na waziri wa mambo ya nje.

Mwezi uliopita, Sultan Qaboos – ambaye hakuwa na mrithi ama mtu aliyekuwa ameteuliwa kuchukua nafasi yake – alikuwa nchini Ubelgiji kwa wiki nzima akipata matibabu na kulikuwa na taarifa kwamba anaugua saratani.

“Kwa huzuni na masikitiko makubwa…familia ya kifalme inaomboleza kifo cha Mfalme Sultan Qaboos bin Said, ambaye alikufa Ijumaa,” taarifa kutoka familia ya kifalme imesema, na kutangaza siku tatu za maombolezo.

Picha zilionyesha kundi la wanaume waliokusanyika nje ya msikiti mkuu wa Sultan Qaboos mji mkuu wa Muscat, ambapo jeneza lake limepelekwa kwa ajili ya maombi maalum.

Kwa kipindi cha miaka 50, Sultan Qaboos ametawala siasa za Oman, nchi yenye idadi ya watu milioni 4.6 huku takriban asilimia 43 wakiwa ni kutoka nchi nyingine.

Akiwa na umri wa miaka 29, Sultan Qaboos alimpindua mamlakani babake, Said bin Taimur, mfalme huyo aliyekuwa na msimamo mkali alipiga marufuku mambo kadhaa ikiwemo kusikiliza redio ama kuvaa miwani ya jua na kuamua nani atakaye oa, kupata elimu au kufurushwa nchini humo.

Mara moja Sultan Qaboos alitangaza kwamba anataka kuunda serikali ya kisasa na kutumia pesa alizopata kwa utajiri wake wa mafuta kuendeleza nchi hiyo wakati ambapo ilikuwa na barabara nzuri ya umbali wa kilomita 10 tu na shule tatu pekee.

Miaka ya kwanza ya utawala wake, kwa usaidizi wa vikosi maalum vya Uingereza, alifanikiwa kukandamiza wanamgambo wa eneo la kusini la Dhofar la watu wa makabila yaliyoungwa mkono na Jamhuri ya Yemen.

Akielezewa kama mtu aliyekuwa na kipaji na maono, Sultan Qaboos aliamua kuchukua msimamo wa kutounga mkono upande wowote katika masuala ya mambo ya nje na alifanikiwa kufanya mazungumzo ya siri na Marekani na Iran mwaka 2013 ambayo yalipelekea kufikiwa kwa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia miaka miwili baadaye.

Hali ya kutoridhishwa na utawala wake ilijitokeza mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la Mapinduzi ya Arabuni.

Oman haikushuhudia msukosuko mkubwa lakini maelfu ya watu walikusanyika barabarani kote nchini humo wakidai mishahara ya juu, nafasi zaidi za ajira na kumalizwa kwa ufisadi.

Awali, vikosi vya usalama vilivumilia maandamano hayo hayo lakini baadaye vikaanza kutumia gesi ya kutoa machozi, risasi za mpira na kufyatua risasi hewani ili kutawanya waandamanaji.

Watu wawili waliuawa na makumi ya wengine wakajeruhiwa.

Pia mamia ya wengine walishtakiwa kwa makosa ya uhalifu, kufanya mikusanyiko ya pamoja kinyume cha sheria na kumtukana sultan.

Hata hivyo maandamano hayo hayakufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa japo Sultan Qaboos alichukua hatua ya kuwaondoa madarakani mawaziri kadhaa waliokuwa wamehudumu kwa muda mrefu kwa madai ya ufisadi, akaongeza nguvu ya Baraza la Ushauri na pia akaahidi kuunda nafasi zaidi za ajira katika sekta ya umma.

Tangu wakati huo, mamlaka imekuwa ikiendelea kuzuia mageziti na majarida yanayojitegemea yanayokosoa serikali, kuchukua kwa nguvu vitabu vinavyoonekana kupinga utawala na kuwanyanyasa wananchi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *