Mrema ameitaka Serikali ya Tanzania kumlipa bilioni 2

Mwenyekiti taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema ameitaka Serikali ya Tanzania kumlipa Sh2 bilioni kama fidia ya kesi alizowahi  kusingiziwa chini ya Serikali ya awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Mbali na fidia pia amemuandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli iliyo na malalamiko yake na kuomba kukutana naye ili waweze kuzungumza juu ya yale aliyofanyiwa na serikali.

Mrema ameyasema hayo leo Jumatano Januari 8, 2020 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya TLP, Magomeni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia hali ya kisiasa nchini tangu awamu ya tatu hadi sasa.

Amesema kwa nyakati tofauti ndani ya uongozi wa Rais Mkapa alisingiziwa kesi ikiwamo ya kumhusisha Rais huyo na rushwa ya Sh500 milioni akiwa katika kampeni za kugombea ubunge wa Temeke mwaka 1996, kutengeneza nyaraka mbalimbali zilizohusisha viongozi wa serikali na tuhuma za rushwa pamoja na kutumia ushahidi wa uongo kushinda kesi.

Amesema kwa sababu Serikali imesema kumbambikia kesi mtu  ni kosa la jinai ambapo wahusika wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani lakini muathirika anatakiwa kulipwa fidia ameomba Rais Magufuli kumlipa fidia kwa niaba ya serikali.

“Kwa kuwa nilibambikiwa na kuzushiwa ya uongo ambayo ni kosa kisheria, nakuomba Rais wa Tanzania (John Magufuli) na serikali yako inilipe Sh2 bilioni kwani haya yote yalifanyika ili kukisaidia chama tawala na serikali yake ili kinishinde kisiasa,” amesema Mrema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *