Mpina ataka Tanzania ijitosheleze kwa uzalishaji wa maziwa

Serikali imeitaka bodi ya Maziwa na Wadau wote wa maziwa kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha ndani ya miaka miwili ijayo Tanzania inazalisha maziwa ya kutosha ili kusiwe na haja ya kuagiza maziwa kutoka nje ya nchi.

Agizo hilo limetolewa  na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina  jijini Dodoma wakati akihitimisha wiki ya Maziwa duniani ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye viwanda vya kusindika maziwa kuongeza uzalishaji zaidi.

Mhe. Mpina amesema kiwango cha kunywa maziwa kwa watanzania kinapaswa kuwa Tani 200 lakini hadi sasa kiwango kinachonyweka ni tani 54 hivyo kuwataka watanzania kuongeza unywaji wa maziwa kwani husaidia kuboresha kinga za mwili na kukuza ubongo

Mhe. Mpina amesema kuwa  ili kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongeza serikali imewaunganisha wawekezaji wa maziwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupatiwa mifugo sambamba pia na kutoa msamaha wa kodi kwenye sekta hiyo.

” Ndugu zangu ni muda sasa wa kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwani Maziwa ni mlo kamili hasa katika kuimarisha mifupa na kuweka ubongo sawa, na yana viini lishe vya kuimarisha pia kinga za mwili”, amesisitiza Mhe. Mpina.

Aidha Mhe. Mpina ameweka wazi kuwa Tanzania ni Nchi ya pili kwa kuwa na Ng’ombe wengi nyuma ya Ethiopia kuwa Tanzania ina  Ng’ombe Milioni 33 lakini Ng’ombe wanaozalisha maziwa ni Milioni 1.9 na kiwango cha maziwa kinachozalishwa ni Bilioni tatu ambacho ni kidogo kulinga na mifugo tuliyinayo.

Mhe. Mpina amesema kwa sasa kuna programu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni kwa baadhi ya mikoa na kusisitiza sasa ni wakati wa kila mkoa kuweka mkakati wa kuhimiza unywaji wa maziwa kwenye kila shule ndani ya mikoa yao.

Pia Mhe. Mpina ametoa wito kwa wawekezaji nchini kutumia fursa ya kuwekeza kwenye usindikaji wa maziwa kwani viwanda vilivyopo kwa sasa vinazalisha asilimia 23 tu ya maziwa na vipo 99.

Mhe. Mpina amehitimisha kwa kuelekeza Halmashauri zote nchini kuzingatia bei elekezi ya chanjo ya mifugo na atakayekaidi hatua kali za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake

Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote amesema wiki ya Maziwa imekua ya manufaa sana kwani wiki hii waligawa Lita 1650 kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.

Dkt. Mrote amesema kuwa ndani ya wiki hiyo ya maziwa walikutana wadau wote wa maziwa na kujadili mambo mbalimbali yatakayoweza kuivusha sekta hiyo ili kufikia hatua ya kuzalisha maziwa mengi na kukuza soko hilo hadi nje ya mipaka ya Nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *