Mpaka wa Namanga ,Holili wafungwa tena

Mipaka miwili ya Tanzania na Kenya eneo la Namanga na Holili imefungwa tena baada ya kuibuka hali ya sintofahamu kuhusu utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa kati ya nchi hizo mbili.

Madereva wa Tanzania wamelalamika kuwa vyeti vyao vimekuwa vikikataliwa wanapoingia nchini Kenya hali inayosababisha taharuki kubwa miongoni mwa madereva wa Tanzania wanaovuka mpaka wa Namanga kuingia nchini Kenya.

Mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe ameeleza kuwa hakuna ushirikiano mzuri walioupata walipokuwa wakifuatialia kilichojiri katika mpaka wa Namanga.

Akiongelea adha wanayopata madereva wa malori wa Tanzania wanapoingia upande wa Kenya Mkuu huyo wa wilaya amesema suala hilo halijatolewa ufumbuzi na serikali ya Kenya ili kuondoa adha hiyo.

”Haiwezekani kwamba dereva amepimwa siku mbili tatu zilizopita kisha anarudia tena kwenda kupimwa eneo jingine kwanza tumeona kitendo hicho ni kitendo cha dharau.”

”Lakini cha pili huwezi kuvunja makubaliano bila kuwa na taarifa zozote za msingi. Alisema Bwana Mwaisumbe.

Kwa sasa hakuna shughuli zozote zinazoendelea, mpaka wa Namanga umefungwa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, kuna magari zaidi ya 500 yaliyoegeshwa Arusha, Longido na mengine Namanga.

Wakizungumza na kituo cha televisheni cha Azam, madereva wa Kenya wamekiri kuwepo kwa changamoto kwa madereva wa Tanzania wanapoingia upande wa Kenya , wakisema kuwa Kenya inakiuka makubaliano.

”Upande wetu wa Kenya hawazingatii kama Tanzania inavyozingatia sisi kwao wanatukubalia kutumia cheti tunachotoka nacho Kenya lakini Kenya hawakubali vyeti vya madereva wa Tanzania wakiingia upande wa Kenya hali hii inatusababisha tuumie sisi sote.” Alisema Joseph Kariuki

Biashara katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Holili pia imekuwa katika hali ya sintofahamu hali ambayo pia imefanya serikali ya mkoa kuingilia kati suala hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa haiwezekani kutokuwa na hali ya usawa katika biashara ambapo ni kinyume cha makubaliano.

”Huenda wiki ijayo mapema tukakaa pamoja kama msimamo wao hautaathiriwa na msimamo wetu wa kukataa madereva wao wasipite pia kwa kuwa hata wao tukiwapima tunawakuta wana virusi.”

”Haiwezekani kwamba biashara ifanyike upande mmoja tu, haiwezekani upande mmoja tu waingie na kutoka halafu huo huo upande ndio utangaze kufunga mpaka, huohuo upande ndio unaotumia mpaka kwa uhuru hapana.”

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa sasa bidhaa za Kenya hazitapita mpakani hapo, na magari yao hayatapita yasiyo na mzigo wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *