Mkwasa ataja sababu ya Yanga kufungwa na KMC

Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amesema kuwa wachezaji wake hawakuwa na utimamu wa kimchezo na kupelekea kufungwa na KMC katika mchezo wa kirafiki.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkwasa amesema kuwa uzembe wa wachezaji wake ulipelekea kupoteza mechi hiyo, huku akiwapongeza KMC kwa mchezo waliouonesha.

“Tumefungwa kutokana na makosa ya uzembe wetu wenyewe, imekuwa ni mechi nzuri kujua matatizo yetu yako wapi ili tuyafanyie kazi”, amesema Mkwasa.

“Niwapongeze wenzetu KMC wamekuwa na mechi nyizgi za majaribio kuliko sisi ambao tuna siku 10 tu hivi sasa, kwahiyo tunahitaji kuongeza nguvu na utimamu wa mwili kwa sababu wachezaji bado hawajapata nguvu ya kutosha”, ameongeza.

Kwa upande wake kocha wa KMC, Habib Kondo amesema kuwa alitarajia kupata matokeo hayo kutokana na kujiandaa vizuri kwani ni mchezo wa tatu kwao wa maandalizi kabla ya ligi kurejea.

Yanga inatarajia kufungua ratiba ya urejeo wa ligi, ambapo itacheza ugenini Juni 13, dhidi ya Mwadui FC mjini Shinyanga, ikiwa ni baada ya Serikali kuruhusu shughuli za michezo kuendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *