Mkuu wa shule ya msingi mayila wilayani kahama mbaroni kwa wizi wa saruji

Watu watatu akiwemo mkuu wa shule ya msingi Mayila iliyopo Kata ya Nyihogo wilayani Kahama mkoani Shinyanga wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za wizi wa mifuko 15 ya saruji katika shule hiyo iliyochangiwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dkt John Pombe Magufuli shilingi milioni tano kwa ajili ya ujenzi.

Watuhumiwa hao walikamatwa jana na jeshi la polisi mjini Kahama ambao ni mlinzi wa Shule ya msingi Mayila, mtunza stoo ambaye ni mkuu wa shule hiyo na mnunuzi wa mifuko hiyo ya saruji wakiwa na mifuko 9 kati ya 15 wanayotuhumiwa kuiba.

Akizungumzia tukio hilo diwani wa Kata ya Nyihogo Shadrack Mgwami amesema baada ya kupokea taarifa ya wizi wa mifuko ambayo ilikuwa imehifadhiwa kwenye nyumba ambayo ipo jirani na shule ya msingi Mayila walikuta mifuko 9 na mifuko 6 ilikuwa imeondolewa.

Amesema baada ya mahojiano na mlinzi wa shule alikiri kuiba mifuko hiyo huku akisema aliagizwa na mtunza stoo ambaye ni mkuu wa shule kuisomba kwenda kuihifadhi katika nyumba hiyo ambapo yeye alilipwa kiasi cha shilingi 15,000 huku diwani huyo akisema katika daftari la vifaa linaonesha hakuna upotefu na limesainiwa na watu wote.

“Baada ya kumuuliza mlinzi kwanini huku hakuna mapungufu kwenye daftari na majibu yake alijibu matumizi ya kutwa nzima kwa mfano mifuko mitatu imetumika walikuwa wanajaza mifuko sita halafu hiyo mitatu iliyoongezwa ndio anaisomba kuitoa stoo”.

Kwa upande wake mkurugenzi halmashauri ya mji wa Kahama Anderson Msumba amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema wananchi wanatakiwa kuendelea kujitolea kuchangia nguvu za ujenzi wa miundombinu ya madarasa na hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa watu ambao wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Aidha kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Joseph Kiyengi amekiri kuwashikilia watuhumiwa hao na upelelezi bado unaendelea na utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *