Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo AJUTIA Kuwaweka Ndani Watumishi Wa Umma bila Kuwasikiliza

Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Mrisho Gambo amekumbushia tukio alilolifanya mwaka 2015/16 akiwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma la kumweka ndani mtumishi pasina kumsikiliza akisema tukio hilo hatolisahau kwani alitumia mamlaka yake vibaya.

Leo Jumapili Novemba 24, 2019 Gambo kupitia ukurasa wake wa Instagram amesema watu wasione siku hizi hawaweki watumishi ndani wakadhani hana mamlaka hapana kwani ametambua kuwa elimu haina mwisho na amekubali kujifunza.

“Nilipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma mwaka 2015/2016, siku moja nilimuagiza Mkurugenzi aniandalie kikao cha ghafla cha watendaji wa vijiji na kata. Kwenye kikao kile watendaji wawili walichelewa kwa zaidi ya masaa 5 nikaagiza wawekwe ndani masaa 24.

“Baada ya saa 24 nikaelekeza waletwe ofisini ili nipate utetezi wao. Mmoja alikuwa ni mtendaji wa Kijiji cha Sibwesa kwenye kata ya Kalya ambako ni Kilomita 422 kutoka makao makuu ya Wilaya ya Uvinza eneo la Lugufu. Mtendaji kwenye maelezo yake aliniambia “ Mkuu nakiri kupokea wito wako wa dharura lakini kwa masaa 6 nisingeweza kuwahi kutokana na umbali wa Km 422 kutoka kijiji kwangu na makao makuu. Kutoka kijijini kwangu ambako ni Barabara ya vumbi lazima nipande pikipiki umbali wa Km kama 30 hivi, halafu nipande Boti kisha nipande basi ndio nipate hiace ya kufika Wilayani. Kwa hakika hata sikupewa nauli na gharama si chini ya laki moja ambayo ni karibu nusu ya mshahara wangu. Lakini kwasababu ya wito wa Mkuu nilitumia gharama zangu binafsi na kukimbazana ili niwe nimetii maagizo yako.


Cha kusikitisha nilipofika tu hata kabla ya kunisikiliza ukaagiza niwekwe ndani saa 24. Akaniambia Mkuu mimi nadhani pale ulinionea na ulitumia mamlaka yako vibaya”. 


“Kwa hakika nilitamani kulia. Nilijisikia vibaya sana. Nilimuomba radhi mtumishi huyu ikiwa ni pamoja na kumrudishia nauli pamoja na mwenzie wa kijiji cha Sibwesa kata ya Kalya.

“Watumishi wetu ni binadamu. Wana changamoto nyingi kama binadamu wengine. Busara ni kuwapa fursa ya kujitetea kabla ya kuwahukumu. Hekima ni kushughulikia changamoto zao kwa kufuata kanuni za utumishi wa Umma. Kupitia kanuni za Utumishi watapata wasaa wa kujieleza kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

“Usione siku hizi siweki watumishi ndani ukadhani sina Mamlaka, siku hizi mamlaka ni Makubwa zaidi kuliko siku za nyuma lakini nimetambua kuwa Elimu haina mwisho na nimekubali kujifunza Uongozi. Nimeamua kujikosoa pamoja na kufanyia kazi maoni ya wanao nikosoa.

“Sisi viongozi vijana bado ni wanafunzi wa Uongozi. Kila siku tunajifunza na kupata uzoefu. Hakika uzoefu ni Mwalimu mzuri!


“Mwaka 2012 niliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mkuu wa Wilaya na kituo cha kuanzia kazi kilikuwa ni Korogwe. Wakati huo nilikuwa Kijana zaidi ya sasa.

“Walimu ni watumishi ninao wapenda sana wakati wote wa Uongozi wangu. Wakati wote wa Uongozi wangu nimekuwa mtetezi wao.

Siku moja nikiwa Wilayani Korogwe nilielekeza niitiwe kikao cha Walimu wote ili niweze kusikiliza changamoto zao ili kwa ushirikiano pamoja na viongozi wenzangu tuzipatie ufumbuzi wa pamoja. Kwenye kikao kile kuna Mwalimu alichelewa na alionekana amekunywa kidogo.

Nikamuuliza, Mwalimu kwanini umechelewa kwenye kikao changu? Akaniambia Mkuu, usinizingue maana mimi nimeshachoka na maisha. Nikamwambia huna adabu na kumuagiza OCD amuweke ndani saa 24.

Kama ilivyo kawaida, kesho yake nikaagiza aletwe ofisini ili nimsikilize.

Nakumbuka Mpendwa Mwalimu aliniambia yafuatayo “ Mkuu, nihurumie mtumishi wako. Jana wakati napata wito wako nilikuwa nimemfumania Mke wangu amelala na mwanaume mwingine kwenye kitanda chetu nyumbani. Sikuona tena thamani ya maisha na nilitamani kujiua. Ili kupotezea nikaona bora nijitundike pombe za kienyeji ili angalau ni-ahirishe matatizo. Wakati nipo njwii ndio napokea simu ya wito wako. Mkuu, Mimi ni wa kusaidiwa na si kuadhibiwa, naomba msamaha”. Huu nao ulikuwa ni mtihani mwingine wa Uongozi kwenye maisha yangu. Ningemsikiliza Mwalimu mapema nina hakika nisinge chukua maamuzi yale.


“Watumishi wa Umma ni TUNU ya Taifa letu. Kabla ya kutumia mamlaka tuliyo nayo ya Masaa 24 hadi 48 tutafakari. Hekima na busara ni sehemu ya Uongozi. Nimeona kwanini Mfalme Suleiman aliomba hekima!”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *