MKE ALIYEFUKUZWA KWA KUTOMPIKIA MMEWE AMCHOMA KISU MME WAKE SHINYANGA

Mwanaume aitwaye Mpemba Gamba (48) mkazi wa Uzogole kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga amejeruhiwa kwa kukatwa na kisu ubavuni na mke wake aitwaye Suzana Richard akilazimisha kurudi kwa mumewe baada ya kufukuzwa sababu za kutompikia mme wake. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema tukio hilo limetokea Aprili 11,2020 majira ya sita usiku katika maeneo ya Uzogole, Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga.
 
“Mpemba Gamba ambaye ni mkazi wa Uzogole akiwa nyumbani alijeruhiwa kwa kukatwa na kisu ubavuni upande wa kulia na mke wake aitwaye Suzana Richard. Chanzo cha tukio ni ugomvi uliotokana na mtuhumiwa kulazimisha kurudi kwa mumewe kwani alifukuzwa siku tatu zilizopita kwa sababu za kutompikia mumewe”,ameeleza Kamanda Magiligimba
Amesema mtuhumiwa alikimbia mara baada ya tukio hilo juhudi za kumtafuta na kumkamata zinaendelea na majeruhi alipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga na kuruhusiwa, hali yake inaendelea vizuri.
 
“Natoa wito kwa wananchi hususani wanandoa na wote walioko katika mahusiano ya kimapenzi waache kujichukulia sheria mikononi bali wafike polisi ofisi za dawati la kijinsia na watoto pale wanapokuwa na migogoro kwenye ndoa zao kwa msaada zaidi wa kusikilizwa na kupatiwa suluhu ya migogoro yao badala ya kujichukulia sheria mikononi”,amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *