Mji wa Kagongwa na Isaka Kahama,Sasa kuanza kupata maji ya KUWASA.

Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira wilayani Kahama mkoani Shinyanga (KUWASA) imesema zoezi la usambazaji wa maji katika mradi wake unaotekelezwa katika Kata za Kagongwa halmashauri ya mji wa Kahama na Kata ya Isaka halmashauri ya Msalala unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya vifaa kukamilika.

Hayo yalielezwa jana Januari 21, 2020 katika kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya mji wa Kahama kuwa mabomba pamoja na mita za bili za maji tayari zimefika ofisi za mamlaka hiyo ambapo kwa sasa zoezi linalofuata ni kuanza usambazaji katika maeneo ya Kata hizo mbili.

Akiwasilisha taarifa hiyo mwenyekiti wa bodi ya KUWASA, meja mstaafu Bahati Matala amesema jumla ya mita 2000 za kusomea bili za maji tayari zimefika ambapo mita 1000 zitaelekezwa katika Kata ya Kagongwa na zingine 1000 zitapelekwa katika Kata ya Isaka halmashauri ya Msalala.

Wakichangia taarifa hiyo katika baraza hilo madiwani Hamidu Kapama wa Kata ya Kahama mjini kupitia chama cha mapinduzi (CCM) amesema licha ya mamlaka hiyo kuendelea kusambaza maji wanatakiwa kuboresha pia huduma zao ikiwemo kuanza kutoa mita za bili ya maji ambazo zitakuwa za ruku kwani wakifanya hivyo itakuwa rahisi mteja anapolipia na fedha yake ikiisha huduma inasitishwa.

Ameongeza kuwa zoezi hilo likifanyika pia litaondoa malalamiko ya wananchi kulipishwa gharama kubwa za maji kwani wasoma mita ya matumizi wamekuwa hawafiki katika makazi ya watu na wanatoa gharama za matumizi kwa makadirio hali inayopelekea baadhi ya wananchi kulalamikia kutozwa gharama kubwa kinyume na matumizi halali ya maji.

Kwa upande wake diwani wa Kata ya Majengo kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Benard Mahongo amesema mamlaka hiyo inapaswa kutambua umuhimu wa madiwani kwa kuendelea kuwapa semina na taarifa mbalimbali za mabadiliko ya bei na taarifa zingine ambazo zinawahusu wananchi na kuacha kusubiria baraza la madiwani pekee kutoa taarifa yao ambapo itakuwa rahisi wao kuwaelimisha wananchi.

Aidha mkurugenzi wa KUWASA Allen Marwa amesema sababu ya gharama za bei ya maji kuwa kubwa wananchi wamekuwa hawalipi kwa wakati na gharama kujilimbikiza hivyo madiwani wazidi kuwaelimisha wananchi kulipa kwa wakati huku akiongeza kuwa usomaji mita unatumika kwa njia ya simu hivyo ndani ya mita tatu kutoka mita ilipo simu inapokea taarifa ya matumizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *