Katika kukabiliana na ubovu wa miundombinu katika soko la Namanga mjini Kahama halmashauri ya Mji huo imeshauriwa kujenga mitaro katika kingo za barabara zinayozunguka soko hilo ili kuyadhibiti maji yanayopita katika barabara hizo na kuharibu miundombinu hiyo.
Hayo yamesemwa mjini Kahama na baadhi ya wananchi waliozungumza na Kahama fm kuhusu changamoto ya mashimo yaliyokuwa katika barabara zinazozunguka soko hilo.
Wamesema kuna mashimo mengi na ya muda mrefu hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara na kuupongeza uongozi wa Kata hiyo kwa kuhamasisha wananchi kuchangia fedha ili kusambaza vifusi vilivyotolewa na halmashauri ya mji wa Kahama kwaajili ya kuziba mashimo hayo.
Diwani wa Kata ya Kahama mjini, HAMIDU JUMA amewapongeza wananchi waliojitolea kuchangia kusambaza vifusi kwenye mashimo hayo na kwamba hali ya miundombinu ya barabara katika soko hilo bado ni changamoto kubwa inayohitaji kutatuliwa.
Barabara nyingi mjini Kahama zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na ubovu na kuziba kwa mitaro hali iliyomlazimu mkuu wa wilaya, ANAMRINGI MACHA kuwaagiza wananchi kuhakikisha wanatoa udongo na taka katika mitaro iliyopo mbele ya Nyumba zao ili kuhakikisha barabara zinakuwa safi.