Mgombea wa chama tawala Everiste Ndayishimye ashinda urais

Tume ya uchaguzi nchini Burundi imemtangaza mgombea wa chama tawala Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika juma lililopita.

Jenerali mstaafu ameshinda kwa 68.72% ya kura zilizopigwa, wakati Agathon Rwasa, kutoka chama kikuu cha upinzani akipata 24.19% ,matokeo yaliyotangazwa na tume hiyo hii leo.

Kwa kuwa Ndayishimiye amepata zaidi ya 50% ya kura, ameepuka kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.

Haya ni matokeo ya awali ya uchaguzi , ambapo matokeo ya mwisho yatatangazwa na mahakama ya kikatiba tarehe 4 mwezi Juni.

Jenerali Ndayishimiye liteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha CNDD-FDD katika kikao kisicho cha kawaida kilichofanyika Gitega, mji mkuu wa kisiasa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu ya chama tawala cha CNDD-FDD.

Bwana Ndayishimiye ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri katika siasa za Burundi walio karibu na Pierre Nkurunziza, ambaye uamuzi wake wa kuwania madaraka kwa muhula wa tatu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ulisababisha mzozo na mgomo wa upinzani.

Wagombea wengine waliochuana kwenye kinyang’anyiro hicho ni pamoja na;

Gaston Sindimwo (Uprona) – 1.64%

Domitien Ndayizeye (Kira Burundi) – 0.57%

Léonce Ngendakumana (FRODEBU) – 0.47%

Nahimana Dieudonné – 0.42%

Francis Rohero – 0.20%

Tangu Jumamosi usiku, siku ya uchaguzi, matokeo ya kura zilizopigwa kutoka wilaya na majimbo mbali mbali nchini humo yalianza kutangazwa.

Kufikia Ijumaa Chama cha Waandishi wa Habari nchini Burundi kilitangaza kuwa mgombea wa chama tawala cha CNDD-FDD anaonekana kushinda kwa kiwango cha 80% kwa asilimia 60% ya matokeo yaliyotolewa katika wilaya

Ushindi wa Bwana Evariste Ndayishimiye ulionekana mapema kulingana na matokeo yaliyokua yakitangazwa kutoka mikoani yaliyotangazwa mwishoni mwa Juma.

Wiki iliyopita Agathon Rwasa, mgombea wa chama cha upinzani cha CNL, alisema: uchaguzi huu ni ‘jambo la aibu’ lililotutokea

Bwana Rwasa aliwaambia waandishi wa habari nchini Burundi kuwa “matokeo ni gishi na hayaaminiki “.

Wiki iliyopita pia Chama cha CNL kilitangaza kuwa kina ushahidi kuwa mgombea wa chama tawala aliibiwa kura.

Wagombea wakuu Evariste Ndayishimiye kutoka kwa chama tawala na Agathon Rwasa wa upinzani , waliomba utulivu huku akisubiri matokeo yanayotarajiwa tarehe 25 mwezi Mei.

Tofauti na uchaguzi uliokuwa ukifanyika miaka ya nyuma , wakati huu ni tume ya uchaguzi pekee yenye uwezo wa kutangaza matokeo.

Bwana Rwasa aliambia waandishi kwamba upinzani unashutumu kukamatwa kiholela kwa zaidi ya wachunguzi kumi katika vituo vya kupiga kura na makosa mengine ya uchaguzi.

Chama chake cha National Freedom Council CNL kilikilaumu wanachama wa chama tawala cha CNDD-FDD kwa udanganyifu unaoshirikisha , kupiga kura zaidi ya mara moja, kupiga kura kwa watu waliofariki pamoja na wakimbizi.

Tume ya uchaguzi au chama tawala hawajatoa tamko lao kuhusiana na madai hayo.

Mitandao ya Twitter, Whatsapp na Facebook ilizimwa nchini humo, wakati wa uchaguzi, BBC ilithibitisha.

Wagombea saba waligombea urais kumrithi Pierre Nkurunziza, hata hivyo wagombea wawili ndio waliopigiwa upatu zaidi, kutoka chama cha upinzani CNL Agathon Rwasa na chama tawala CNDD-FDD Evariste Ndayishimiye.

Siku ya leo inakamilisha utawala wa bwana Nkurunziza ambaye aliingia madarakani katika taifa hilo la Afrika Mashariki miaka 15 iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *