Marekani yakana kumiliki ndege iliyodunguliwa Afghanistan

Awali, maafisa wa eneo hilo walisema kwamba ndege iliyoanguka katika eneo la Deh Yak, jimbo la Ghazni, inamilikiwa na shirika la ndege la serikali la Ariana.

Hata hivyo, shirika hilo limekanusha taarifa hii na kuzua maswali kuhusu mmiliki halisi wa ndege hiyo na chanzo cha ajali.

Shirika la habari la Iran la Fars limeweka kwenye mtandao video iliyosema kuwa ni ndege yenye alama za jeshi la anga la Marekani.

Video na picha katika mitandao ya kijamii ya shirika la Fars, inaonesha kile kinachoonekana kama ndege ya kivita ya E-11A, ya jeshi la anga la Marekani.

Jeshi la Marekani linatumia aina hii ya ndege kwa upelelezi wa angani, Afghanistan.

Kijiji ambacho ndege hii imeanguka, kusini magharibi mwa mji mkuu Kabul, ni eneo lenye idadi kubwa ya kundi la Taliban.

Jenerali Beth Riordan, msemaji wa makao makuu ya jeshi, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, amesema bado haijafahamika ndege iliyopata ajali ni ya kina nani.

Afisa mwengine wa jeshi la ulinzi la Marekani, ameliambia gezeti la Military Times kwamba “Tunafahamu taarifa hizo na tunafanya uchunguzi wetu. Hadi kufikia sasa hatuwezi kuthibitisha kuwa ndege hiyo ni ya jeshi la ulinzi.”

Awali, ndege hiyo ilishukiwa kwamba ni ya shirika la ndege la Ariana lakini baadaye shirika hilo likakanusha vikali madai hayo na kusema wakati huo ilikuwa na ndege mbili pekee angani na kwamba zote ziko salama.

Mirwais Mirzekwal, mkurugenzi wa shirika la Ariana, ameliambia shirika la habari la Reuters: “Ndege iliyoanguka sio ya shirika la Ariana kwasababu ndege mbili zinazomilikiwa na Ariana zilizokuwa zinatoka Herat kuelekea Kabul na kutoka Herat kuelekea Delhi ziko salama.”

Gavana wa eneo la Ghazni, Wahidullah Kaleemzai baadaye alizungumza na shirika la habari la kibinafsi la TOLOnews: “Bado hakuna taarifa kamili kuhusu waliojeruhiwa wala jina la ndege iliyoanguka.”

Bodi ya anga ya Afghanistan pia imesema kwamba hakuna ndege yoyote ya abiria ilioanguka, na msemaji wa kundi la Taliban Zabihullah Mujahid ameiambia BBC kuwa kundi lake bado halina taarifa za ndege ilioanguka.

Kamanda wa polisi wa Ghazni, Ahmed Khalid Wardak, ameiambia BBC hakuna taarifa kuhusu waliokuwemo kwenye ndege hiyo na kwamba haifahamiki ni nini kimesababisha ajali hiyo.

Aliongeza kuwa aidha ndege hiyo imeshika moto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *