KAHAMA:Jamii yaaswa kuwaogesha mabinti dawa ya Mvuto “Nsamba”

JAMII katika Kanda ya Ziwa,imekemewa juu ya dhana potofu ya kuwaogesha dawa za mvuto wa mapenzi “ Nsamba”,watoto wao wa kike kwakuwa tabia hiyo inachangia uwepo wa ndoa na mimba za utotoni na kusababisha kukatisha masomo kwa mabinti zao.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,Neema Katengesya,alikemea tabia hiyo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika jana,viwanja vya Shule ya Msingi Segese,vilivyo Halmashauri ya Msalala.

Katika maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Shirika la C-SEMA chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na idadi ya watu (UNFPA),Katengesya alisema jamii ya Kanda ya Ziwa imekuwa na uroho wa mali kiasi cha kumfanya mtoto wa kike kitega uchumi.

Alisema kutokana na kurithi tabia hiyo toka kizazi na kizazi wamekuwa na kasumba ya kuwapeleka watoto wa kike kwa Waganga wa Kienyeji kuoshwa dawa za mvuto wa mapenzi ili wapate kuolewa mapema na kutoona umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.

“ matokeo ya tabia hiyo,ni ongezeko la mimba za utotoni na watoto wa kike kukatisha masomo,hali hii haikubaliki kwani inamnyima haki ya kielimu binti,”alisema.

Katengesya alizidi kukemea suala hilo kwa kuiasa jamii kumpa fursa sawa mtoto wa kike kama ilivyo wa kiume kwakuwa ana haki zake,pia anaweza kuongoza kwa umahiri katika jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini,Dkt.Amiri Batenga,alisema maendeleo ya dunia yanahitaji mchango mkubwa wa mtoto wa kike katika kutatua changamoto mbalimbali.

Hivyo alisema ni vyema jamii kumlinda mtoto wa kike kusudi asipoteze ndoto zake,na kubainisha tayari Shirika lake kwa kushirikiana na C-SEMA pamoja na Serikali wanahakikisha wanamlinda mtoto wa kike kwa kumpatia elimu ya kujitambua na kujithamini kusudi afikie malengo yake.

 

Nae Mgeni wa heshima katika Kilele hicho,mwanamitindo Nancy Sumari,aliwaasa mabinti kuwa jasiri kwa kuepuka na kuvikataa vitendo ambavyo vinahatarisha kufikia ndoto zao huku wakiishika elimu ambayo ni mkombozi wa maisha yao.

Bi Sumari aliwaomba watoto wa kike kutokata tamaa katika safari ya masomo kutokana na kutoka katika familia duni za kimaisha na kuwasihi changamoto hizo za kimaisha ziwe fursa za kuwafikisha katika kilele cha mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *