KAHAMA:Basi la Frester Lasababisha kifo cha mtoto mmoja na kujeruhi wengine 23.

Mtoto mmoja ambaye hajafahamika jina wala Makazi mwenye umri unaokadiriwa kuwa ni miaka 7 amefariki dunia na wengeine 23 kujeruhiwa katika ajali ya basi Kampuni ya Frester linalofanya safari kati ya Kahama – Musoma lenye namba za usajili namba T 965 DST lililokuwa likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina mara moja aliyetoka baada ya kusababisha ajali hiyo.

Ajali hiyo imetokea leo  majira ya saa 12 asubuhi muda mfupi baada ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini Wilbroad Mtafungwa kulikagua basi hilo na kuruhusiwa kuendelea na safari ambapo lilipofika katika eneo la Nyakato nje kidogo ya mji wa kahama lilipindika kutokana na mwendokasi bila ya kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

Kamanda Mtafungwa  Amesema kuwa kabla ya kuanza Safari kwa mabasi yote yaendayo mikoani alikukutana na Madereva hao na kuwakumbusha kuhusiana na kuzingatia sheria  za Usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha kwa mwendo kasi na kuzingatia alma za barabarani.

“Dereva huyu ni mzembe haiwezekani upatiwe elimu ya Usalama barabarani halafu muda huo huo ukiuke sheria na kusababisha ajali kwa uzembe,ambayo imesababisha ajali kwa watu zaidi ya 23 na kusababisha kifo cha mtoto mmoja,tutachukua hatua kali dhidi yake pindi atakapokamatwa,”alisema Mtafungwa.

Ameongeza kuwa basi hilo lilikuwa na abiria 47 ambapo 23 wamejeruhiwa watatu hali zao sio nzuri huku wengine wakiruhusiwa kuendelea na safari baaada ya kupata michubuko ambapo kampuni hiyo ililazimika kuwatafutia usafiri mwingine na kuendelea na safari yao ya kuelekea Musoma mkoani Mara.

Kasiani Msaki ni mmoja wa Majeruhi wa ajali hiyo amesema kuwa Dereva wa basi hilo alikuwa anaendesha kwa mwendokasi ambapo alipofika eneo la tukio alishindwa kulimudu gari hilo wakati akilikwepa gari dogo lililokwa mbele yake ndipo lililopo teleza na kuingia mtaroni na kupinduka.

“Dereva wa basi hili alikuwa anafanya mashindano na mabasi mengine,tunaimba serikali ichukue hatua kali dhidi yake,amesababisha kifo na ulemavu kwa watu bila sababu ya msingi kwa kushindwa kuchukua tahadhari licha ya kupatiwa elimu na maafisa wa Usalama barabarani,”alisema Msaki.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha amezitaka Mamlaka zinazosimamia Usalama barabarani kuhakikisha wanachukua hatua kali za kisheri Madereva ambao ni wazembe kwa kufungia leseni zao ili waweze kujifunza umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

“Haiwezekani tuendelee kuwavumilia madereva wa mabasi wanaoendelea kufanya mashindano barabarani huku wakiwa na abiria,tutatuchua hatua kali kwao ili kudhibiti ajali zinasababisha vifo kwa watu wasiokuwa na sababu na kupunguza nguvu kazi ya Taifa,”alisema Macha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *