KAHAMA: CRDB Kanda ya Magharibi yatoa msaada wa madawati Shule ya Sekondari Kitwana.

Benki ya CRDB kanda ya magharibi imetoa msaada wa viti na meza  88 katika shule ya Sekondari Kitwana Wilayani Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni muendelezo wa kusherehekea wiki  ya huduma kwa wateja iliyoanza Jumatatu Octoba 5 mwaka huu.

Akipokea msaada huo mkuu wa wilaya ya kahama Annamringi Macha ameishukuru benki ya CRDB kwa kujitoa mara kwa mara kuchangia miradi ya maendeleo na kuziomba taasisi zingine kuiga mfano wa CRDB.

Macha ameongeza kuwa msaada huo wa viti na meza umepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo katika shule ya Sekondari Kitwana  licha ya kwamba mwakani halmashauri  ya mji wa kahama ina mzigo mkubwa kutokana na wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza kuwa wengi kuliko mwaka huu.

Kwa upande wake Meneja biashara wa benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Jumanne Wagana amesema kuwa msaada huo wa viti na meza umegharimu Shilingi milioni saba na kwamba Benki ya CRDB itaendelea kutoa misaada ya kijamii kupitia asilimia moja ya Faida wanayoitenga kila mwaka.

Sambamba na hayo Wagana ametoa wito kwa wadau na wananchi mbalimbali kuitembelea benki ya CRDB ili kujifunza mengi na kufungua Akaunti mbalimbali kupitia wiki ya huduma kwa wateja.

Naye meneja wa CRDB Tawi la Kahama Evod Kereti amewaasa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitwana kuwa kuna akaunti maalumu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ambayo kufungua ni bure na kwamba wakawaambie wazazi wao ili waweze kuwafungulia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kitwana Flora Cleopa Mwanri amewaomba wadau wa elimu kupitia Ofisi ya mkuu wa wilaya kusaidia upatikanaji wa Bweni la wasichana ili kuwaepusha mabinti na vishawishi vya ngono pamoja na kuwafanya wazingatie masomo.

Awali akisoma Risala mkuu wa Shule ya Sekondari Kitwana Basil Kijazi ameishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo na kuongeza kuwa kwa sasa kinachowakabili ni thamani za walimu kwani walimu wanatumia viti na meza za wanafunzi.

Benki ya CRDB imeendelea kusaidia misaada mbalimbali ya kijamii ikewemo Afya na Elimu kupitia asilimia moja ya Faida wanayopata kila mwaka katika matawi yake yote nchini.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *