JK ataja mambo 9 Nyerere kukumbukwa

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ametaja mambo tisa ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, atakumbukwa na viongozi wanapaswa kuyaiga na kuyaishi.

Kikwete alitaja jambo la kwanza la kumkumbuka Nyerere kuwa ni ukombozi wa nchi. Alisema Nyerere alisimama mstari wa mbele kuhakikisha ukombozi wa nchi unapatikana kutoka kwa wakoloni.

“Kwa maono yake ya mbali alipopewa uongozi wa TANU, kila walivyokaa na kujadili maslahi, walibaini siasa za kuwaletea watu uhuru na kuamua kuundwa Tanu na yeye kuwa Rais.

“Kwa vile, hawakuruhusiwa kufanya kazi na siasa, akaamua kuchagua kuacha ualimu Pugu na kupiga siasa isiyokuwa na mshahara. Kazi yake ikawa kuzunguka kudai uhuru ambao hakuwa na uhakika kama utapatikana na kama utapatikana, utapatikana lini. Kwa moyo wa upendo kwa wenzake alijitoa kwa ajili ya maslahi ya wengi.

Alilitaja jambo lingine kuwa ni utayari wa kujitoa. Katika hilo alisema Nyerere aliacha kazi yenye mshahara kwa matumaini kuwa nchi ikipata uhuru Watanzania wote watafanikiwa. Alisema Nyerere amewafundisha kuwa na moyo wa tayari kujitolea kwa maslahi ya wengi.

Kikwete alitaja jambo la tatu la kukumbukwa ni Watanzania wamshukuru kwa karama alizopewa kwa kuendesha harakati za kudai uhuru kwa maneno na kupatikana kwa maneno bila kumwaga damu.

“Usione vinaelea vimeundwa. Ni maarifa na uhodari wake ndinyo uliotufikisha hapa. Wako wenzetu haikuwezekana hili walilazimika kutumia nguvu,” alisema.

Alitaja jambo la nne kuwa ni imani ya haki na umoja kwa kushirikiana na Abeid Amani Karume kuanzisha taifa la Tanzania jambo ambalo ni urithi mkubwa.

“Hii ni moja ya tunu ya taifa ambayo haikuwapo kwenye ramani lakini wameitengeneza Nyerere na Karume. Wako wengine Afrika wamejaribu ikashindikana. Namibia imeshindikana, sisi tumeweza na tuna miaka 55 sasa na tuna miaka 155 ijayo tutakuwapo,” alisema.

Jambo la tano alilitaja kuwa ni ujenzi wa taifa lenye umoja, amani na mshikamano miongoni mwa raia.

“Nchi yetu ina makabila 120, dini mbalimbali. Wapo ambao walikuwa hawajaegemea upande wowote si Wakristo si Waislamu. Kwa sasa tuna vyama vya siasa mbalimbali bado nchi ina amani. Kuna matajiri na maskini, wapo wasomi na maprofesa, wapo wasiojua kuandika lakini bado wote wanaishi pamoja.

Wenzetu wana makabila mawili na dini moja imeshindikana,” alisema.

Jambo la sita , alilitaja kuwa ni kuheshimu utu wa mtu. Alisema pamoja na ukubwa wote aliokuwa nao kama Rais, alikuwa wa kawaida mbele ya wengine na alikuwa anakaa na kuhusiana na watu.

“Ulikuwa ukikaa naye hupati hofu kwamba umekaa na Rais. Ni mtu ambaye alikuwa anaweza kusema weka ndani, ukawekwa ndani lakini Mwalimu hakua hivyo. Alikuwa mnyenyekevu, mpole lakini si kwamba yuko hivyo basi ukagonge naye mkono. Huwezi kufanya hivyo, alifanya hivyo akisisitiza utu na dhamana ya uongozi” alisema.

“Dhamana ya uongozi haikufanyi wewe uwe mtu zaidi ya mwingine yeyote aliyepo pale, haikufanyi wewe kwamba uwe na haki zaidi kuliko mtu mwingine ambaye si kiongozi. Ni jambo kubwa kwa viongozi kutambua kwamba kujishusha hakukufanyi usiwe kiongozi. Ukiwa na wanadamu wenzako ujue nao ni wanadamu kama wewe,” alisisitiza.

Kikwete alitaja jambo la saba kuwa Mwalimu aliamini uhuru wa Tanganyika hauna maana kama bado hata nchi moja ya Afrika itakuwa bado imetawaliwa ndiyo maana alihakikisha kudai uhuru wa nchi mbalimbali.

“Jambo la nane, Mwalimu Nyerere aliwapenda vijana na alitambua umuhimu wa kuwalea na alikuwa karibu na Umoja wa Vijana. Alitupatia fursa ya kuanza kujifunza uongozi si wa juu. Kuanzia chini, tulijifunza kusema, kutoa mawazo na kujifunza kutambua jinsi nchi inavyoendeshwa,” alisema.

Jambo la tisa, alisema Mwalimu Nyerere aliamini katika meza ya mazungumzo na kutolea mfano mwaka 1988, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) walifanya maandamano kupinga wabunge kujiongezea mishahara.

Alisema katika maandamano hayo, kulisambazwa makaratasi yenye hoja ya kisiasa ya vyama huru vya siasa, vyama huru vya wafanyakazi na uhuru wa kugoma.

“Kama kawaida Nyerere alikuwa akiongoza nchi na chama. Katika kikao cha Kamati Kuu (ya CCM) tulijadili tukio hili kubwa. Mwalimu alisema pamoja na hayo kulikuwa na makaratasi haya nataka msome wote halafu tutayarishe majibu.

“Tukasoma tukamaliza tukasema huu ni uhaini wakamatwe watiwe kizuizini. Mwalimu Nyerere akasema mawazo hayapigwi rungu, mawazo yanashindwa na mawazo yaliyo bora zaidi. Maadam wamejenga hizi hoja sisi hoja zetu ni zipi,” alihoji.

“Nyerere ametuachia urithi wa mambo mengi muhimu. Katika nyanja zote za maisha ya Watanzania ni wajibu wetu kuutambua na kuudumisha na baadhi yake yameshakuwa tunu la taifa,” alisisitiza.

Kikwete aliwataka Watanzania, viongozi wa CCM na vyama vingine vya siasa, makabila, madhehebu yote washikamane katika kusimamia tunu hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *