Jeshi la Polisi Lafanikiwa Kumtia Mbaroni Aliyemuua Mkewe Kwa Kumkata na Shoka

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kumkamata muimba kwaya Moses Pallangyo (28), aliyemuua mke wake Mary Mushi, kwa kumkata na shoka kichwani, katika kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru na kwamba baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo amekiri kufanya mauaji hayo.
Akizungumza leo Disemba 29, 2019, Kamanda wa Polisi mkoani humo Jonathan Shanna, amesema kuwa jeshi hilo lilimsaka mhalifu huyo kwa kutumia kikosi cha Mbwa ambacho ndicho kilichofanikisha kumkamata, akiwa mafichoni kuelekea nchini Kenya.
“Jana Disemba 28 saa 11: 30 jioni, tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo, ambaye tuliahidi kumtafuta kwa namna yoyote ile na ‘Dog Style’ ndiyo imeleta mafanikio ya kumkamata yaani ilikuwa bandika bandua, mtuhumiwa tumemhoji kwa kina na amekiri kufanya kitendo hicho cha kikatili, na tulitaka kujua kwanini amefanya kitendo hicho akasema ni shetani alimpitia” amesema Kamanda Shanna.
Tukio hilo lilitokea Disemba 25, 2019 majira ya mchana, jambo ambalo hapo awali lilihusishwa na ugomvi wa kifamilia ikiwemo wivu wa mapenzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *